January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati mpya wanafunzi wanaopata ujauzito kurejea shule

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeweka mkakati mpya kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito kuwawezesha kuwaendelea kimasomo. Anaripoti Mwanaharusi Abdallah, TUDARCo … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdullah Juma.

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaendeleza kimasomo watoto wa kike waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito,” ameuliza Asha.

Akijibu swali hilo, Kipanga amesema, serikali imeweka mikakati kwa wanafunzi walokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo wasichana walopata ujauzito wakiwa masomoni.

Kipanga ambaye pia ni Mbunge wa Mafia amesema, mikakati hiyo ni pamoja na mpango wa elimu nje ya mfumo rasmi.
“Katika mfumo huo wanafunzi wataruhusiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne na kidato cha sita na kwa sasa kuna vituo 753 vya elimu nje ya mfumo rasmi ambavyo vimesambaa katika mikoa yote Tanzania,” amesema Kipanga.

Hata hivyo, amesema serikali imeendelea kutoa fursa kwa wanafunzi walopata ujauzito wakiwa masomoni kujiendeleza kimasomo na fursa hivyo ni pamoja na Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Waliokosa (MEMKWA), mpango wa elimu kwa vijana uitwao elimu changamani kwa vijana walio nje ya shule (integrated programme for out of school adolescents-IPOSA).

Pia amesema, serikali imetoa fursa ya kujiendeleza kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDC) ambapo husisitiza katika kujifunza taaluma, stadi za ufundi wa awali, ujasiriamali na stadi za maisha.

Msingi wa swali hilo, unatokana na katazo la Serikali lililotolewa mwaka 2017 la kupiga marufuku kwa wasichana waliopata ujauzito wakiwa masomoni kuendelea na masomo.

Zuio hilo liliibua mjadala mkali kwa wadau mbalimbali wakiitaka Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanarejea masomoni baada ya kujifungua kwani kuwazuia linakwenda kinyume na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu na pia ni kumnyima msichana haki yake ya msingi ya kupata elimu.

Akiuliza swali la nyongeza, Asha ameuliza “jambo hili ni zito, linavuruga usichana wao na maisha yao na linavuruga familia, je serikali haioni ni muda mwafaka kuwarejesha shule baada ya kujifungua kwani mimba si maradhi ya kuambukizwa.”

Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Pia ameuliza “Je, serikali haioni kuzuia watoto wa kike kuendelea na masomo yao na kuwaachia watoto wa kiume kuendelea na masomo huoni huo ni ubaguzi?

Baada ya maswali hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amemuita Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kujibu swali hilo akisema, ndani ya mwaka mmoja wanatekeleza utaratibu huo.

“Sasa ndiyo tunaanza kutekeleza mpango mahusisi, tutekeleze japo kwa mwaka mmoja kuona utakavyokuwa wakati serikali inaendelea kutafakari cha kufanya,” amesema

Katika swali la pili, Profesa Ndalichako amesema “mwaka 2016, Bunge lilitunga sheria ambayo inatoa adhabu kali kwa mtu anayejihusisha na mapenzi shuleni ikiwemo anayempa ujauzito mwanafunzi. Yoyote anayebainika anapata adhabu ya kifungo cha miaka 30.”

Mara baada ya majibu hayo, Spika Ndugai ameutaka Mtandao wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) “kulichukua hili kama mkakati wenu wa miaka mitano. Nafikiri hatuhitaji kusema, waziri anajua Watanzania wanataka nini.”

error: Content is protected !!