March 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati kumvua Lissu ubunge wavuja     

Spread the love

MKAKATI wa kumvua ubunge, Mwasheria Mkuu wa Chama cha Demokarsia na Maendeleo (CHADEMA) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, sasa umeiva. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya Bunge na serikalini mjini Dodoma zinasema, mkakati huo unaoratabiwa na baadhi ya vigogo wandamizi kutoka ndani ya serikali, umepangwa kutekelezwa wakati wowote kwenye mkutano ujao wa Bunge.

Bunge la Jamhuri limepanga kuanza mkutano wake wa Nane, tarehe 2 Aprili mwaka 2019. Pamoja na mengine, mkutano huo utajadili bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2019/2020.

“Hili la kumfuta Lissu ubunge tayari limeiva. Linaweza kutekelezwa wakati wowote katika mkutano ujao wa Bunge,” ameeleza mtoa taarifa wetu.

Anasema, “tayari vikao kadhaa vimefanyika kwa lengo la kuchambua sheria za Bunge, Kanuni na taratibu nyingine ambazo zitatumika kulimaliza jambo hili.”

Kwa mujibu wa taarifa hizo, hatua ya kutaka kumvua Lissu ubunge, inatokana na kitendo cha mwanasiasa huyo kuzunguuka ulimwengu “kuichafua serikali.”

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja takribani siku 10 tangu Lissu mwenyewe kudai kuwa Bunge la Jamhuri limepanga kumvua ubunge wake.

Alisema, ameelezwa kuwa hoja itakayotumika kumvua ubunge wake, ni madai ya kushindwa kuhudhuria vikao kwa muda mrefu na kwamba taarifa hizo amezipata kutoka kwa watu wawili tofauti.

“Kwamba, sijamwandikia barua Katibu wa Bunge na sijampata taarifa yoyote ya maandishi kuhusu kuumwa kwangu wala matibabu yangu na kwamba sijahudhuria vikao vya Bunge tangu tarehe 7 Septemba 2017,” ameeleza Lissu.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya ilikanushwa na Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai, ambaye alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akisema, hana taarifa wala hajui kuwapo kwa mkakati huo.

Kwenye waraka wake, Lissu alisema, sababu za kushindwa kuwasilisha taarifa za maandishi, hazina msingi. Alipelekwa Nairobi akiwa mahututi na viongozi wote wa Bunge walikuwa na taarifa ya kile kilichompata.

Aidha, kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja wiki moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuliambia Bunge kuwa suala la Lissu linahitaji kuangaliwa kwa upekee.

Alisema, “ni kweli kwamba Lissu hayupo jimboni. Hayupo bungeni, hayupo nchini  na hayupo hospitalini na wala mimi sina taarifa yake yoyote wala ya daktari wake. Wala mwenyewe hahangaiki kunijuza wapi alipo.”

Ndugai alikuwa akijibu mwongozo ulioomba kwake na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma aliyadai kuwa Lissu anazurura duniani huku akidai anaumwa.

Alihoji: “Kwa nini Bunge lisisitishe mshahara wake kwa sababu ameshapona na ameendelea kuzunguuka huko na huko akitukana Bunge na Serikali?”

Ndugai alisema, “hoja yako ina msingi. Iko haja ya kusimamisha mishahara wake. Na nikuhakikishie kuwa yale yaliyo ndani ya uwezo wangu nitayafanya.”

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, yuko nchini Ubelgiji anakopatiwa matibabu kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein, kufuatia kushambuwa kwa risasi nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma, tarehe 7 Septemba 2017.

Alikwenda Ubelgiji, tarehe 6 Januari mwaka jana. Kabla ya kwenda Ubelgiji, Lissu alipata matibabu kwenye hospitali ya mkoa wa Dodoma na Nairobi.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni Lissu ameonekana akizunguuka dunia na kufanya mahojiano na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, akiituhumu Serikali ya Rais John Pombe Magufuli, kuminya uhuru wa kujieleza na kuvunja misingi ya kidemokrasia nchini.

Katika ziara zake hizo, Lissu ameendelea “kumwaga sumu,” katika nchi kadhaa Ulaya na Marekani kwa kusisitiza kuwa shambulio dhidi yake, “lilipangwa na kutekelezwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya viongozi serikalini.”

Amesema, “nimeambiwa na watu ambao sina shaka na maneno yao, kwamba mtu mmoja mwenye madaraka makubwa alitaka nife. Aliagiza nikifa…hakuna shughuli bungeni na nisiletwe nyumbani kwangu Dar es Salaam. Nikimbizwe kijijini kwetu nikazikwe as soon as possible (haraka iwezekanavyo).

Lissu anasema, taarifa hizo ameelezwa na baadhi ya marafiki zake walioko ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Haya nimeyapata kutoka ndani ya serikali,” anasema Lissu na kuongeza, “pamoja na kwamba wapo watu waliotaka nife, lakini hiyo haina maana kwamba sina marafiki. Ninao wengi, tena wengine ni mawaziri na viongozi wandamizi ndani ya chama tawala.”

Anasema, “ndio hao walioniambia wameshindwa kuja Nairobi kuniona. Walambiwa kupitia kwenye kikao, hii habari ya Lissu msiishabikie na tena msithubutu kwenda Nairobi.”

Katika hatua nyingine, serikali imemtaka Lissu kurejea nyumbani ili kushiriki kile inachokiita, “uchunguzi wa kushambliwa kwake.”

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Arusha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema kuwa Lissu ndio muhusika mkuu wa tukio hilo na kwamba serikali inashindwa kuendelea na uchunguzi kutokana na kutokuwepo kwake.

Alisema, serikali inapata kigugumizi kuendelea na uchunguzi huo kutokana na kukosekana kwa baadhi ya mashahidi muhimu kwenye tukio hilo.

Lugola amesema, Lissu katenda tukio ambalo halijawahi kutokea nchini na kuita hatua yake ya kuwapo nje ya nchi, ni kutelekeza kesi yake.

Akahoji: “Kwa nini hataki kurudi nchini?” Akaongeza: “aache kuwaeleza wazungu, kwa sababu wanaopeleleza kesi siyo wao.”

Akijibu madai hayo, Lissu amesema, hana haja ya kuogopa kurejea Tanzania.

“…watulie kidogo, wanazungumza as if (kama vile) mtu hataki kurudi. Hakuna mtu aliye-miss Bunge kama mimi na ndio maana nawaambia wale wanaotaka nirudi.

“Leo watulie kwanza, maana madaktari wangu hawajasema nimepona; ila wamesema ninaweza kunyoosha miguu Ujerumani, Uingereza na Marekani, bado sijapona.”

Kuhusu madai ya kukwama kwa uchunguzi wa tukio lake, Lissu anahoji, “kama ningekufa, uchunguzi usingefanyika? Hayo maneno wakawaambie watu ambao hawafahamu maana ya uchunguzi. Siyo Watanzania wa leo.”

error: Content is protected !!