Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mjadala katiba mpya wapamba moto
Habari za Siasa

Mjadala katiba mpya wapamba moto

Spread the love

 

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC), kimeendesha mdahalo wa wazi kujadili ufufuaji wa mchakato wa katiba mpya. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mjadala huo umefanyika leo Jumatano tarehe 21 Aprili 2021, kwa njia ya mtandao, na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo; Mwanazuoni, Dk. Azaveli Lwaitama na mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk. Ananilea Nkya.

Mchakato wa Katiba Mpya ulioanza mwaka 2011 chini ya uongozi wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, uliahirishwa 2 Aprili 2015, kwa kura pendekezwa kutokana na uandikishaji wapiga kura uliokuwa ukifanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutokamilika.

Kura hiyo ilikuwa ifanyike tarehe 30 Aprili 2015. Tangu wakati huo, mchakato umekuwa kimya na haijafahamika utaaanzia lini.

Leo Jumatano, akifungua mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, amesema kituo hicho kimechukua hatua hiyo ili kushawishi mchakato wa katiba hiyo uliokwama kwenye utawala wa Kikwete ueanze.

“LHRC tangu tuanze mwaka 1995 tumekuwa tukitoa elimu kuhusu utawala wa sheria na haki za binadamu na utawala bora. Tuna amini, maendeleo yanahitaji uwepo wa katiba inayoheshimu haki, utawala wa sheria na katiba,” amesema Henga

“Ukiangali kila tatizo la mfumo wa utawala, chanzo chake ni katiba, unakuta imeacha pengo au kuna tatizo. Katiba mpya tunaona ni jawabu tosha katika kuimarisha utawala bora wa sheria na haki za binadamu.”

Akichangia hoja katika mchakato huo, Askofu Shoo, ameshauri mchakato huo utakapofufuliwa, usiishie njiani kama ilivyokwama mchakato uliopita, huku akishauri elimu kuhusu umuhimu wa katiba, itolewe kwa wananchi.

“Kwa hiyo, ni muhimu badala ya kusema tufanye viraka viraka itakuwa shida, tumesikia Katiba ya 1977 imefanyiwa marekebisho mara 14, bado tunaona kuna mapungufu makubwa, kwa hiyo lengo langu sasa mchakato huo ufanyike bila kukwama,” amesema Askofu Shoo.

Naye Dk. Lwaitama amesema “wale watakaohusika na mchakato rasmi wa upatikanaji katiba mpya, ni lazima watu wasiwe na masilahi na mchakato huo.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda amesema, marekebisho ya katiba hiyo ni ya muhimu kwa kuwa katiba iliyopo ina mapungufu katika kuainisha masuala ya utawala bora, sheria na haki za binadamu.

“Katika mjadala unaohusu utawala bora, sheria na haki za binadamu, tunaona kuna mapungufu ya msingi katika Katiba iliyopo, dhana hizi hazijawekwa bayana. Nadhani wanaohitaji Katiba mpya wana hoja ya msingi sababu katiba hii haijakidhi dhana hizi tatu,” amesema Mbunda.

Kwa upande wake, Dk. Ananilea Nkya amesema “tunahitaji Katiba mpya itakayotoa usawa wa kijinsia katika uongozi, pamoja na kupungunza mamlaka ya rais hususan katika kuteua viongozi wa wilaya na mikoa.”

Ananilea Nkya

“Katika nchi nyingine, ukitaka ufanye vizuri, mtu akitaka kupewa kazi ya umma, atafanyiwa interview (mahojiano), ataangaliwa hekima yake na uzoefu wake, sababu anatumikia wananchi,” amesema Dk. Nkya, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).

“Viongozi wetu sasa hivi, hawafanyi kazi kwa sababu ya Jamhuri, wanafanya kazi kwa sababu ya waliowateua, kuangalia kama watawaona kwenye uteuzi,” amesema Nkya.

Rehema Maro, akichangia kwenye mjadala huo, ameshauri elimu juu ya marekebisho ya Katiba itolewe kwa wananchi, ikiwemo mapungufu ya katiba ya sasa na hoja zinazokwenda kujengwa katika kuipata Katiba mpya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!