BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limeagiza kurudiwa upya kwa mitihani iliyovuja ya utabibu ndani ya wiki sita kuanzia tarehe 1 Novemba, 2021. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Pia limeagiza mitihani hiyo kufanyika sambamba na mitihani ya marudio (Supplementary Examinations) kwa programu zingine za afya nchi nzima.
Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma tarehe 4 Novemba, 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Aifello Sichalwe wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema Wizara ya Afya inawaagiza wakuu wa vyuo vyote vya afya kuwapa taarifa wanafunzi ili wajiandae kwa ajili ya mitihani hiyo.
Aidha, amesema Wizara imesikitishwa udanganyifu wa mitihani uliotokea lakini pia amesema itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki kufanya udanganyifu huo.
Pia amewataka wanafunzi wa vyuo kuzingatia masomo na kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu kwani vina madhara makubwa kwao na kwa jamii.
“Tunaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa ipo makini na itatumia jitihada zote kulinda usalama wao” amesema.
Amesema Wizara ya Afya ina jukumu la kutunga, kusimamia na kutathmini Sera na miongozo mbalimbali ikiwemo ya rasilimali watu katika Sekta ya Afya nchini.
Amesema Wizara inatambua umuhimu wa rasilimali watu wenye weledi na umahiri kwa ajili ya usalama wa afya za wananchi.
“Mitihani ya muhula wa pili kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ilifanyika kitaifa kuanzia tarehe 16 Agosti, 2021 hadi 30 Septemba, 2021.
“Siku ya mwisho ya ufanyikaji wa mitihani ya nadharia, Wizara ilipokea taarifa ya kuwepo kwa viashiria vya kuvuja kwa mitihani hiyo na hivyo kulazimika kuunda Kamati ya uchunguzi iliyojumuisha Wataalamu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
“Kamati hiyo imefanya uchunguzi kuanzia tarehe 6 Septemba, 2021 hadi tarehe 17 Oktoba, 2021 ilipowasilisha taarifa ya awali katika uchunguzi huo.
“Kamati imebaini kwamba mitihani ya mwaka wa pili (NTA level 5) ya Programu ya Utabibu (Clinical Medicine) ilivuja, lakini mitihani ya Programu zingine zote haikuvuja,’ amesema.
Aidha, amesema wakati wa uchunguzi wa mitihani iliyovuja, kamati ilibaini mitihani hiyo ilisambazwa kupitia mitandao ya kijamii (telegram na WhatsApp) na kuonekana kwenye baadhi ya namba za simu za wanafunzi zilizofanyiwa uchunguzi na Kamati.
Katika hatua nyingine amesema wanafunzi hao walipohojiwa walikiri kupata mitihani hiyo kupitia makundi ya mitandao ya kijamii yaliyoanzishwa na wanafunzi hao kwa ajili ya kujadiliana.
Amesema Kamati ya uchunguzi imewasilisha taarifa ya uchunguzi ambayo imethibitisha kuwepo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya vyuo vilivyochunguzwa kupitia namba za simu za wanafunzi.
Aidha, Mganga mkuu ameeleza kwamba uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watu, vyuo na taasisi zingine zilizojihusisha na udanganyifu huo.
Amesema taarifa hiyo iliwasilishwa kwenye Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) tarehe 24 Oktoba, 2021 kwa ajili ya maamuzi kwani ndicho chombo cha kisheria chenye mamlaka na vyuo vya elimu ya kati nchini.
“Katika kikao cha 78 cha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kilichokaa tarehe 1 Novemba, 2021 taarifa hiyo ilijadiliwa, kupitia Sheria ya
Baraza Sura 129 na Kanuni za Mitihani, Kifungu 33 (1) (iii), 2004 (GN.75) limefuta matokeo ya mitihani ya nadharia (theory) kwa masomo yote ya Programu ya Utabibu Ngazi ya Tano (NTA Level 5)” ameeleza.
Leave a comment