November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mitaala ya Elimu Tanzania kufumuliwa tena

Prof. Joyce Ndalichako

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania iko mbioni kufanya maboresho ya mitaala ya elimu ya msingi, vyuo vya kati na ufundi stadi pamoja na vyuo vikuu , ili ikidhi matakwa ya mazingira ya sasa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, tarehe 18 Juni 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, katika mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu uboreshaji mitaala ya elimu ya awali, msingi na sekondari, jijini Dar es Salaam.

“Katika karne ya 21, dunia imeshuhudia mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia, yaliyoleta utawandazi ambayo moja ya athari zake ni kuongezeka ushindani katika soko la ajira,”

“ Na katika muktadha huo, kuna umuhimu mkubwa kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi na maarifa yatakayowezesha kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira, kujiajiri, kuajirika na kumudu maisha yao kila siku,” amesema Prof. Ndalichako.

Aidha, Prof. Ndalichako amesema, mabadiliko ya mitaala hiyo yatajikita katika kuweka stadi zitakazowezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kutumia sayansi na teknolojia, ili kwenda sambamba na utekeleza wa sera ya sasa ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.

“Kwa kuzingatia kuwa nchi yetu imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda, tunahitaji kuwa na wahitimu wabunifu wanaoweza kutumia sayansi na teknolojia, kubuni vyanzo zaidi vya kukuza na kuimarisha uchumi wa Taifa letu,” amesema Prof. Ndalichako.

Wakati huo huo, Prof. Ndalichako ameziagiza taasisi za elimu ya juu, kuanzisha mijadala kwa ajili ya kujadili namna ya kuboresha mitaala yao.

“Natoa wito kwa taasisi za elimu ya juu nchini, suala hili halihusu elimu ya msingi pekee. Linahusu pia elimu yetu ya kati na vyuo vya elimu ya juu, niwaelekeze taasisi za elimu ya juu muanzishe mijadala kama hii ya kupitia mitaala yenu, kupata maoni kwa wadau,” amesema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema mabadiliko hayo yatakuwa ya sita, tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1964.

Amesema mabadiliko ya kwanza ya mitaala yalifanyika 1967, ambayo yalilenga kuondoa mitaala ya kibaguzi iliyowekwa na wakoloni, kisha kuweka mitaala ya kujenga uzalendo kwa kuzingatia falsafa ya ujamaa na kujitegemea.

Mkurugenzi mkuu wa Tasisi ya Elimu Tanzania, Dk. Aneth Komba

Waziri huyo wa elimu amesema, mabadiliko ya pili yalifanyika 1979, yaliyolenga kuweka msisitizo kwenye elimu ya nadharia na vitendo.

“Mabadiliko haya ya mitalaa yalilenga kuweka msisitizo kwenye elimu ya nadharia na vitendo, hivyo masomo ya michepuo yalianzishwa rasmi. Ikiwemo mchepuo wa ufundi, kilimo na sayansi kimu. Nadharia hizi zilianzishwa kujenga stadi zitakazowezesha wahitimu nchini kujikwamua kiuchumi kutokana na falsafa hiyo,” amesema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema, mabadiliko ya tatu yalifanyika 1997, yaliyozingatia matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 1995 na Tume ya Kufanya Mapitio ya Elimu iliyoongozwa na Hayati Jackson Makweta 1982.

Amesema mabadiliko ya nne yalifanyika 2005, ambayo yaliweka mkazo kwenye ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia ujenzi wa umahiri, ikiwemo kuanzisha somo la Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Pamoja na uchopekaji wa masuala ya mtambuka kama vile elimu ya Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) na stadi za maisha na mazingira.

Prof. Ndalichako amesema, mabadiliko ya mwisho yalifanyika 2014, ambayo yanatumika kuanzia 2015 hadi sasa.

“2014 mabadiliko makubwa yalifanyika katika mitaala, yalilenga zaidi katika ngazi ya mwanzo ya wanafunzi. Yalilenga katika kuboeresha ufundishaji mitaala ngazi ya awali na msingi. Msisitizo uliwekwa kujenga ujuzi na kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesbau maarufu KKK,” amesema Prof. Ndalichako.

error: Content is protected !!