July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Misuli ya Lowassa yatetemesha CCM

Watia nia Bernard Membe (kushoto) akisalimiana na Edward Lowassa leo asubuhi katika kikao cha Halmashauri Kuu

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi kimeingia katika wakati mgumu kimaamuzi baada wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kugomea matokeo yaliyotoka ya Kamati Kuu kuchagua majina matano lakini huku wakimtupa nje Edward Lowassa. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Ile tu kuwakaribisha wazee wastaafu wa chama – wakiwemo marais na wenyeviti wa chama, makamu wenyeviti wa chama, kulisikika mvumo tofauti na ilivyo kawaida.

Katika kufuatilia matangazo ya moja kwa moja yanayorushwa na AZAM TV kutokea mjini Dodoma, ilishuhudiwa sauti ya baadhi ya wajumbe kuimba wimbo maalum wa chama wa kukaribisha viongozi wakubwa, na wakalichomeka jina la Lowassa pale palipotakiwa jina la Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete.

Wakati hali ikichafuka ukumbini, mwanasiasa mkongwe na aliyepata kuwa mjumbe wa muda mrefu wa Kamati Kuu, Kingunge Ngombale-Mwiru, alisema lipo tatizo ndani ya Kamati Kuu kwa kuwa tayari baadhi ya wajumbe walilalamika yametolewa kuwa utaratibu umekiukwa.

Wazee wastaafu walioingia ukumbini na kukabiliana na tafrani hiyo ni marais na wenyeviti wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, makamu wenyeviti Amani Karume, John Malecela, Cleopa Msuya, Pius Msekwa na waziri mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim.

 

Wimbo uliomtukuza Lowassa kwa kusema “tuna imani na Lowassa” haukusimama hata alipokuwa anaingia ukumbini mwenyekiti Kikwete, ambapo alishuhudia kisicho cha kawaida kikiendelea.

 

Taarifa zilizopatikana baadaye, zimesema baada ya ufunguzi wa kikao, ulioandamana na mwenyekiti kusoma ajenda za kikao ikiwemo ya kuchagua majina ya wagombea watatu ya kupelekwa mkutano mkuu, kuliibuka zogo kuwa wajumbe wamekosa imani na maamuzi ya Kamati Kuu na kutaka ivunjwe.

Bila ya shaka zogo hilo lilifuatana na msingi wa hoja ulioanza jana kwa wajumbe watatu wa Kamati Kuu – Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa – walioeleza wazi mbele ya waandishi wa habari kuwa hawakukubaliana na maamuzi yale hasa kwa kuwa kanuni zimekiukwa.

Walisema kanuni inataka Kamati Kuu ipokee majina ya waombaji wote na kuchagua watano baada ya kufanya uchambuzi; hayo matano ndiyo yatapelekwa NEC. Dk. Nchimbi alisema nje ya ukumbi baada ya kamati kuu kumaliza kikao usiku, kwamba kamati ilipokea majina machache.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye leo ameyathibitisha majina yote matano ambayo gazeti hili la MwanaHALISIOnline liliyachapisha jana usiku.

Waliopitishwa ni Balozi Amina Salum Ali, January Makamba, Dk. Asha Rose-Migiro, Dk. John Magufuli na Bernard Membe. Nape aliwaambia waandishi wa habari majina hayo ndiyo yatafikishwa NEC kupigiwa kura ili kutoa majina matatu yatakayopelekwa Mkutano Mkuu utakaochagua jina moja usiku huu.

Haijajulikana mpaka sasa majina mangapi hasa yalifikishwa Kamati Kuu. Kama yote 38 yalipokewa, kama wengine walikatwa na Kamati ya Usalama na Maadili baada ya mahojiano au kamati kuu iliyakata baadhi ya majina.

Zogo kubwa lililozuka ukumbini na kusababisha kikao kuvurugika kwa wajumbe kutakiwa kutoka nje kwa mapumziko kwa nusu saa, lililenga kushinikiza mabadiliko ya maamuzi, wakati tayari mwenyekiti Kikwete alishasihi wajumbe wawe watulivu na waache jazba kwa kuwa “ukiwa na jazba hoja zako hazitasikika.”

Mapumziko yalichukua saa nzima kabla ya wajumbe kuitwa kurudi ndani ambako ajenda ya mwisho ya tano ilikuwa ianze. Hii ni ajenda ya kuchagua majina matatu ya kupelekwa mkutano mkuu ili kutokana nayo, wajumbe wachague mmoja atakayetamkwa kuwa ndiye mgombea wa CCM atakayeshindana na wagombea wa vyama vingine kutaka ridhaa ya wananchi kuongoza taifa.

Wakati hayo yakitokea ukumbini, kwenye uwanja wa Nyerere Square, uliopo ng’ambo ya majengo ya makao makuu ya CCM, kundi la wanachama lilikuwa limekusanyika, huku wakiimba na kupiga mayowe ya kumtakia Lowassa arudishwe kwenye uteuzi kwa kuwa ndiye tumaini lao.

Ngombale-Mwiru amesema yaliyotokea kwenye kamati kuu ni mambo yaliyojengewa mazingira mapema lakini anasikitika kuwa matokeo yake yatakivuruga chama katika wakati muhimu kinapohitajika kuwa na “mshikamano ili kipate mgombea mzuri anayekubalika ndani ya chama na nje ya chama.”

Mwanasiasa huyo ambaye amejitokeza hadharani kumuunga mkono Lowassa katika harakati za kutafuta uteuzi wa kugombea urais, alikuwa anahojiwa na mtangazaji wa Azam TV, Charles Hillary mjini Dodoma.

Amesema ni muhimu viongozi wakuu wa CCM wakakumbuka kuwa mteuliwa atakayepatikana ndiye atakuwa mgombea atakayesimama kushindana na wagombea wa vyama vingine kuwania urais. “Akishinda na kuwa rais huyu ndiye atakuwa mwenyekiti wa chama chetu, atakuwa amiri jeshi mkuu wa taifa letu. Je katika hawa watano walioteuliwa kwa sasa wanazo sifa za kubeba bendera ya chama chetu.”

Mahojiano na watu mbalimbali waliopo kwenye viwanja vya makao makuu ya CCM yameonesha kwamba wengi wa washabiki wa chama hicho hawakupendezwa na uamuzi wa kamati kuu kumkata Lowassa.

Mpaka sasa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kinaendelea ili kupata majina matatu.

error: Content is protected !!