MIRADI ya uwekezaji 294 yenye thamani ya Dola za Marekani 8.12 bilioni (Sh. 18.75 trilioni), imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2022. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 10 Machi 2022, jijini Dodoma na Waziri wa Uwekezaji, Dk. Ashatu Kijaji, katika mkutano wake wa kuelelezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa kipindi cha mwezi Machi 2021 hadi Februari 2022, Serikali ya Awamu ya Sita imevutia na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294, yenye thamani ya Dola 8.129 bilioni sawa na Sh. 18.75 trilioni,” amesema Dk. Kijaji.
Waziri huyo wa uwekezaji, amesema kwa mujibu wa takwimu za uwekezaji za 2020/2021, thamani ya miradi hiyo imeongezeka kutoka Dola 1 bilioni hadi 8.129 bilioni, ambayo itatoa ajira kwa Watanzania 62,301.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na ushawishi kwa Rais Samia kwa wawekezaji, pamoja na makongamano ya biashara ya ndani na nje ya nchi, ambayo Serikali yake imeshiriki, ikiwemo la uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya, lililofanyika Mei 2021.
Leave a comment