January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mimi ndiye rais wenu – Maalim Seif

Spread the love

KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad amewaasa wananchi wa Unguja na Pemba kutambua kuwa chama hicho ndicho kilichopata ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 na wasihadaike na propaganda za viongozi wa CCM. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Maalim Seif ambaye ndiye aliyegombea urais kupitia CUF amesema kwamba yeye ndiye anayestahili kutangazwa mshindi na atatangazwa wakati wowote mgogoro ukishamalizika.

Alitoa kauli hiyo leo alipokuwa akihutubia viongozi wa chama hicho ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na kamati tendaji za wilaya za Unguja kwenye ukumbi wa Majid Store, Mombasa mjini hapa.

Amesema mazungumzo yake na Jakaya Kikwete kabla ya kuondoka madarakani yalikuwa mazuri na yaliyokuwa ya kina na kufikiwa makubaliano huku akimuachi kuamilisha kazi iliyobakia rais mpya, Dk. John Magufuli.

Amesema kwamba dunia nzima inajua ukweli wa kwamba Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi ameshinda uchaguzi mkuu wa Zanzibar isipokuwa CCM ikaamua kupindua ukweli huo kwa maslahi binafsi ya kung’ang’ania madaraka.

Maalim Seif amesema wana CUF na Wzanzibari wote bila ya kujali tofauti zao za kisiasa na nyinginezo watulie wakiamini kuwa watatangaziwa rais wao halali na si mwingine baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kukamilisha uhakiki wa matokeo ya mwisho ya majimbo 23 yaliyobakia wakati Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha “alipokurupuka na kutangaza peke yake kuyafuta matokeo ya uchaguzi wote.”

“Mimi sina wasiwasi ninajihesabu kama Rais wa

Zanzibar ninayesubiri kuitwa na kuapishwa, na sasa nimo katika matayarisho ya kuunda serikali ili nikiapishwa tu nisipoteze tena muda wa kufikiria kuunda serikali,” amesema katika kikao cha kwanza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.

Amesema Tume wanachokifanya ni kuchelewesh tu utaratibu wa kukamilisha kazi yao ya wajibu kwa mujibu wa Katiba ya Zanibar, 1984, lakini akasema, “nina uhakika, wataikamilisha na kutangaza matokeo yaliyo halali kwa sababu kila mtu anayajua kwa sasa.”

Wakati akisema hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi inayofanya kazi za Mwenyekiti wa chama hicho baada ya kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba, amesema CUF haina fikra hata chembe za kuwepo uchaguzi mpya kwa Zanzibar baada ya ule wa Oktoba 25 ambao Wazanibari walishuhudiwa wakimpa ridhaa Maalim Seif Shariff Hmad ya kuongoza nchi yao.

Twaha Taslima ambaye ni mwanasheria na wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania amesema Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) la CUF limeridhia kwamba chama hicho kimeshinda uchaguzi na limelaani njama za kumtangaza mtu asiyechaguliwa na wananchi.

Taslima amesema njama hizo zimeongozwa na Mwenyekiti Jecha akitumiwa na wanasiasa wahafidhina wa Chama Cha Mapinduzi wanaoshindwa kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kutaka kung’ang’ania madaraka.

Bado alisema Baraza lina imani kuwa Tume itakamilisha kazi ya kuhakiki matokeo ya majimbo 23 yaliyobakia na “kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo aliyechaguliwa kihalali ambaye atakuwa ni Maalim Seif Shariff Hamad.”

Wakati huohuo, mwanasheria gwiji nchini aliyeongoza timu iliyoandika Katiba ya Zanzibar mwaka 1980, Aboubakar Khamis Bakary ametangaza rasmi kuwa mawaziri wote katika serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein wanaotoka CUF wameshakabidhi ofisi na gari serikalini.

Aboubakar ambaye alikuwa akiongoza wizara ya Katiba na Sheria, amesema wametekeleza hatua hiyo ya kisheria baada ya uongozi wa serikali ya Dk. Shein kumaliza muda wake rasmi ilipofika Novemba 2 mwaka huu.

Alisema kwa mujibu wa Kif. 28 cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Rais Dk. Shein alikamilisha muhula wa miaka mitano tarehe hiyo na mtu yeyote anayetafsiri vinginevyo katiba, anafaa kuitwa “mbumbumbu wa sheria.”

“Mimi ni mwanasheria na mtaalamu hasa wa masuala ya katiba na hakuna wa kunidanganya. Wanaosema rais Dk. Shein anaongoza kihalali eti kwa kuzingatia kifungu cha 28, hawajui wanachokifanya, au wanapotosha makusudi ukweli ili kukidhi matakwa yao binafsi,” amesema Aboubakar.

Amemsihi Dk. Shein azingatie katiba badala ya kusikiliza viongozi wa CCM ambao alisema wanatafuta njia ya kutengeneza mgogoro mwingine wa kisiasa Zanzibar baada ya kushindwa uchaguzi.

“Lazima tufike mahali tuithamini demokrasia tuliyoamua kuijenga. Haikubaliki kuwasumbua wananchi wa Zanzibar kwa uchaguzi ambao baadhi yetu wanasiasa hatuko tayari kupoteza madaraka, hii si sahihi hata kidogo,” amesema gwiji huyo wa sheria aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali ya Zanzibar baada ya Zanzibar kupata katiba yake ya kwanza tangu ile iliyovunjwa na Mzee Abeid Amani Karume mwaka 1964 yalipofanyika mapinduzi.

Oktoba 28 mchana, ndipo Mwenyekiti wa ZEC, Jecha alitangaza kwenye eneo ambalo halijaelezwa vizuri ni wapi, kuufuta uchaguzi wote wakati mwenyewe alishatangaza matokeo ya urais katika majimbo 31, kati ya 54 ya Zanzibar. Wakati huo tayari fomu za matokeo yote zilikuwa zimebandikwa kwenye kuta za vituo vya uchaguzi nchini kote.

Alichukua hatua hiyo inayoelezwa kama ya shinikizo kutoka uongozi wa juu wa CCM, siku mbili baada ya Maalim Seif kutangazia ulimwengu kuwa alikuwa na kura asilimi 52.87 dhidi ya 47.13 za Dk. Shein, na kutaka Tume isicheleweshe matokeo.

Pia alimsihi Dk. Shein kukubali matokeo hayo na kutoa ushirikiano kama alivyokubali yeye katika uchaguzi mkuu wa 2010. Alisema atashirikiana na CCM kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kama Katiba inavyoelekeza.

error: Content is protected !!