SERIKALI ya Tanzania, imetumia zaidi ya Sh. 800 milioni kukarabati Chuo cha Ualimu Bustani kilichopo Kondoa mkoani Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi tarehe 18 Juni 2020 na Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia aliyembelea chuo hicho kuangalia uboreshaji wa miundombinu.
Profesa Ndalichako amesema, Serikali imetoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu kwa kurabati, kujenga miundombinu ya taasisi za elimu ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuboresha dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji.
Kuhusu ukarabati na ujenzi unaoendelea kwenye vyuo vya ualimu, Profesa Ndalichako amasema, serikali inaboresha miundombinu ya vyuo hivyo kwa awamu ambapo awamu ya kwanza imehusisha vyuo 10, awamu ya pili vyuo 8 na awamu ya tatu vyuo tisa na chuo cha Bustani kikiwemo na kufanya idadi kufikia 27 kati ya 35 nchini nzima.
“Huu ni uwekezaji mkubwa ni vizuri miundombinu hii ikatunzwa kwa sababu serikali inatumia fedha nyingi kurudisha hadhi ya vyuo hivi.”
“Fedha iliyoletwa katika Chuo cha Ualimu Bustani Februari ni Sh. 874 milioni kwa ajili ya kukarabati na kuongeza majengo mapya ambayo ni bweni, nyumba za walimu ikiwemo ya mkuu wa Chuo na kuongeza baadhi ya majengo kama Hosteli za wanafunzi wa kike,” amesema Profesa Ndalichako
Ametumia fursa hiyo, kuwataka wanafunzi kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao, kujitambua na huku wakiilinda tunu za Taifa zilizoachwa na waasisi wa nchi hii.
“Vijana uzalendo ni pamoja na kueleza mazuri yanayofanywa na serikali yenu, hata haya yanayofanyika hapa chuo cha Bustani, myaseme kwani hali ya miundombinu kabla ya ukarabati na baada ni tofauti sana ni jukumu lenu kueleza mafanikio ya serikali ndani ya Taasisi zenu na hata nje,” amesema Profesa Ndalichako
Pia, ametumia fursa hiyo kuwatakia kila lakheri walimu tarajali wa mwaka wa pili wanaokwenda kuanza mitihani ya elimu ya ualimu tarehe 29 Juni 2020.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makota ameishukuru serikali kwa namna ambavyo inapelekea miradi katika halmashauri ya Kondoa na hasa Chuo cha Ualimu Bustani na ujenzi wa ofisi za uthibiti Ubora wa Shule.
Amesema, miaka miwili iliyopita wizara ilipelekewa mradi wa maji ambao umekua msaada mkubwa kwenye chuo hiko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha ualimu Bustani, Joina Chanafi amemueleza Profesa Ndalichako chuo hicho kina jumla ya watumishi wakufunzi 31 na kwamba hali ya utoaji elimu katika chuo hicho inaendelea vizuri bila changamoto yoyote.
Chanafi ameishukuru Serikali kwa kukarabati miundombinu ya chuo hicho ili kurejesha hadhi yake lakini pia kukiletea chuo kwa wakati fedha za uendeshaji ugharamiaji wa maji, chakula na umeme.
Leave a comment