KIASI cha Sh.750 milioni, zimepangwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Kiegeani wilayani Mafia, mkoani Pwani, na kwamba tayari ujenzi wa kituo hicho umeanza rasmi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Akizungumza wakati wa kuzindua ujenzi huo wiki iliyopita, mkuu wa wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo amesema, tayari eneo lote linalotarajiwa kufanyika ujenzi limesafishwa.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya amesema, mbali na kusafisha eneo hilo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limehamisha njia ya umeme na baadhi ya makaburi yaliyokuwa ndani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kipya.
Kwa mujibu wa Mhandisi Ntemo, kati ya fedha hizo, Sh.500 milioni zimetolewa na serikali kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi (Results Based Finance – RBF).
Fedha hizo, zitatumika kwa ajili ya kujenga jengo la wazazi, jengo la upasuaji, nyumba mbili za watumishi na jengo la kufulia.
Kiasi kingine cha Sh.250 milioni, zilizopokelewa kupitia tozo ya simu, zitatumika kujengea jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara na kichomea taka.
Amesema, mpaka sasa, tayari matofali 27,278 kati ya 40,000 yanayohitajika, yamefyatuliwa na misingi ya majengo hayo umekamilishwa.
Ujenzi wa kituo hicho umeanza Oktoba 2021 na umepangwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Mhandisi Ntemo alitoa maelezo hayo, wakati akizungumza na wakazi wa maeneo jirani na kituo hicho waliofika kushuhudia uzinduzi huo.
Alitumia mkutano huo wa uzinduzi, kuwaasa vijana kujitokeza kushiriki katika kazi ambazo zimepangwa kutekelezwa kwa kutumia nguvu za wananchi.
Alisema, halidhishwi na muitikio wa wananchi hasa vijana katika kuchangia mradi huo.
Amesema, waliokuwa mstali wa mbele kujitolea nguvu kazi, ni watu wenye umri mkubwa, jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa jamii inayolenga kujiletea maendeleo yake yenyewe.
“Tunatarjajia kuwa vijana ndio wanufaka wakubwa wa huduma hii, sasa inapotokea ushiriki wao unakuwa wa kusuasua inatia shaka, endapo vijana hawa wanaelewa dhamana waliyonayo juu ya mustakabali wa maendeleo ya kisiwa cha Mafia,” alieleza DC Ntemo.
Alisema, “dunia haisimami. Hivyo wakati tunafanya mzaha kwa shughuli muhimu kama hizi, mtambue wazi kuwa wenzetu wanatuacha kwa mbali.”
Mkuu huyo wa wilaya amesema, hatavumilia ucheleweshaji wowote wa mradi huo ambao ameutaja kuwa ukombozi kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Leave a comment