July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mikopo ya Kilimo nje nje TADB

Spread the love

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria kusaidia upatikanaji wa masoko ili kuongeza mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini, anaandika Saidi Mkabakuli.

Dhamira hiyo inalenga kufanya mabadiliko kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Akizungumzia katika Warsha ya Kitaifa ya Wadau ya Sekta ya Kilimo katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam, Thomas Samkyi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, amesema kuwa kukosekana kwa masoko ni moja ya changamoto kuu zinazorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Kwenye warsha hiyo yenye mada kuu isemayo: ‘Wazalishaji Tuanze na Soko,’ Samkyi amesema serikali iliamua kuanzisha TADB ili kusaidia kutokomeza changamoto hiyo na nyinginezo.

Sababu kuu ni kusaidia kukabiliana na upungufu huo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo na masoko katika sekta ya kilimo na hatimaye kuleta mapinduzi katika kilimo nchini.

“Katika kutekeleza majukumu yetu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imeanza huduma zake kwa kulenga minyororo michache ya ongezeko la thamani katika kilimo.

“Mikopo ya aina mbalimbali hutolewa kuwezesha wakulima kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini,” amesema Samkyi.

Kwa mujibu wa Samkyi, TADB inatoa mikopo kwa ajili ya uwekezaji kwenye ujenzi, viwanda vya kusindika mazao, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya usindikaji wa mahindi.

Pia ununuzi wa vifaa vya uvunaji wa kisasa wa mahindi, vifungashio vya kisasa vya kuhifadhia mahindi na teknolojia ya uhifadhi wa mahindi kupunguza upotevu wa mazao.

“Kwa sasa tumejikita katika mnyororo mzima wa uongezaji wa thamani kuanzia uandaaji wa shambani hadi kwa upatikanaji wa masoko, ikiwemo mahitaji ya uzalishaji wenye tija kwenye sekta nzima ya kilimo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba.

“Kupima ubora wa udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye uzalishaji wa mahindi, upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea, madawa na vifaa na teknolojia mbali mbali za umwagiliaji na fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uzalishaji wa mahindi,” amesema.

Samkyi ameongeza kuwa benki imejipanga kutoa mikopo ya ununuzo wa mitambo na mashine za ukaushaji, usafishaji na uchambuzi wa madaraja ya mahindi.

Pia mitambo ya usindikaji na usagaji wa nafaka na ujenzi wa viwanda vya kusindikia mazao ikiwamo fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uendeshaji katika kuongeza thamani ya mazao.

Amesema, benki inatoa mikopo kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kilimo katika kuimarisha minyororo ya thamani katika kilimo.

“Inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na mitambo ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima vya maji ya umwagiliaji, ujenzi wa mabawa ya uvunaji maji ya mvua, ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mahindi na ujenzi wa miundombinu ya masoko,” amesema.

Robert Pascal, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo amesema kuwa benki inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni mikopo ya muda mfupi (miezi 24), mikopo ya muda wa kati (miaka miwili hadi mitano) na mikopo ya muda mrefu(miaka mitano hadi 15).

“Riba itozwayo kwa upande wa mikopo ya muda mfupi ni asilimia saba 7 mpaka 8 kwa mwaka. Mikopo hii hutolewa kwa ajili ya kufanikisha shughuli za kilimo kwenye mnyororo wa thamani,” amesema.

error: Content is protected !!