September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mikoa ya Korosho yaongezwa

Spread the love

 

BODI ya Korosho Tanzania imeongeza mikoa ya uzalishaji wa zao hilo sambamba na kuongeza wabanguaji wadogo, anaandika Christina Haule.

Mikoa iliyoongezwa katika uzalishaji korosho ni Morogoro, Dodoma, Singida na baadhi ya maeneo yenye joto katika Mkoa wa Iringa.

Lengo ni kuongeza uzalishaji na upatikanani wa korosho kwa wananchi kufuatia asilimia 90 ya korosho ghafi inayozalishwa nchini kuuzwa nje ya nchi kisha bidhaa kurejeshwa na kuuzwa kwa bei ya juu.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mangile Malegesi, Kaimu Meneja wa Tawi la Dar es salaam, Bodi ya Korosho Tanzania kwenye maonesho ya wakulima 88 Kanda ya Mashariki (TASO) yanayofanyika kikanda katika Kata ya Tungi mkoani Morogoro.

Malegesi amesema, asilimia 90 ya korosho ghafi zinauzwa nje ya nchi na kufanya wakulima kukosa korosho za kubangua na kwamba, zinaporejeshwa bei yake inakuwa juu.

Amesema, zao hilo lilizoeleka kulimwa katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Tanga na Pwani.

Malegesi amesema, kufuatia kuongeza maeneo ya kilimo kwa ajili ya kukuza uzalishaji, wanatarajia kuongeza uzalishaji na kuzalisha tani laki 5-6 ifikapo mwaka 2019 ambapo mwaka 2015 walizalisha tani laki 1.5.

Amesema, ili kwenda sambamba na ongezeko hilo la uzalishaji, bodi hiyo inatarajia kuweka mpango wa ubanguaji wa korosho katika makundi makuu matatu wakiwemo wabanguaji wadogo, wakati na wakubwa.

Amesema, jambo litakalosaidia korosho kubanguliwa kwa wingi na kupunguza bei yake pale itakapomfikia mlaji.

Amesema, tayari wameunda vikundi vya ubanguaji katika Halmashauri za Kibaha, Tandahimba, Masasi na Ruagwa ambavyo wanavipa elimu sambamba na kuvikabidhi mashine kwa ajili ya kuanzisha ubanguaji mdogo.

error: Content is protected !!