July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Migogoro ya ardhi yapatiwa ‘mwarobaini’

Spread the love

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imezindua mchakato wa kujenga mfumo unganishi wa taarifa za ardhi kwa njia ya mtandao wa inteneti (ILMIS), ambao unatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi, anaandika Pendo Omary.

Mfumo huo ambao pia utahusisha upigaji picha wa jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa ramani ya jiji, unatarajia kuanza kufanya kazi Wilaya ya Kinondoni, kisha wilaya zote za mkoa wa Dar na badaye katika kanda zingine.

William Lukuvi, waziri wa wizara hiyo, akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo amesema, “mfumo huu utatuwezesha kuwa na uhakika wa kupata kwa haraka taarifa za wamiliki halali wa viwanja na kupunguza au kumaliza migogoro inayohusu viwanja kutolewa mara mbili.”

Lukuvi amefafanua kuwa, chini ya mfumo huo haitakuwa rahisi kwa mtu kughushi nyaraka za umiliki wa viwanja, ambavyo nyaraka zake zimepotea na kutambua maeneo yaliyopagwa kwa shughuli maalum ili kudhibiti udanganyifu katika sekta ya ardhi.

“Mfumo huu, utatoa uhakiki wa usalama wa nyaraka mbalimbali za sekta ya ardhi na kuwezesha ufuatiliaji wa matumizi bora ya ardhi na chini ya utekelezaji wa miradi huu, wizara yangu itaboresha huduma za upimaji kwa kila kanda.
“Tutanunua vifaa vya upimaji wa kisasa vitakavyosambazwa katika kanda nane tulizonazo,” amesema Lukuvi.

Dk. Yamungu Kayandabila, Katibu Mkuu wa wizara hiyo amesema, serikali imeamua kujenga mfumo huo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya taarifa za sekta ya ardhi ambalo limesababisha uwepo wa hitaji la mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na mfumo wa kufuatilia pango la kodi ya ardhi.

Katika kutekeleza matakwa ya mfumo huo, kampuni ya IGN FI imepewa zabuni ya kuhakikisha mfumo unaudwa vyema huku kampuni ya COWI ikipewa zabuni ya kupiga picha jiji la Dar es Slaam ili kusaidia uchoraji wa ramani ya kisasa.

error: Content is protected !!