July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Migogoro ya ardhi Morogoro kukoma

Spread the love

HATUA ya kukomesha migogoro ya ardhi mkoani Morogoro imeanza kuchukuliwa baada ya wataalam watano kutoka Tume ya Taifa inayosimamia migogoro ya ardhi nchini kuwasili, anaandika Christina Raphael.

Timu hiyo iliyo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasili mkoani humo ili kukamilisha kazi ya upimaji ardhi ikiwa ni hatua za awali kudhibiti mapigano kati ya wakulima na wafugaji yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara.

William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema hayo leo wakati akizungumza kwenye kikao kilichojumuisha viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.

Lukuvi amesema, timu hiyo itakayoongozwa na Dk. Steven Nindi, Mkurugenzi Mkuu mpya wa tume hiyo ambapo itashughulika na kuhakiki mipaka ya vijiji sita ambavyo vina migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji na kusababisha maafa wilayani humo.

Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni vile vinavyozunguka Bonde la Mpunga la Mgongola ambavyo ni Hembeti, Dihombo, Mkindo Sindoni, Mkindo kwa Boma, Kambala na Kikundi.

Aidha amesema kuwa, timu itachukua muda mrefu katika zoezi hilo ambapo pia itaandaa mipaka ili kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Hata hivyo aliwataka wataalamu hao kuhakikisha wanaainisha maeneo kwa kufuata mipaka ya vijiji kwa mujibu wa sheria ili kukomesha migogoro hiyo.

error: Content is protected !!