May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mifumo ya ukusanyaji mapato kufumuliwa

Charles Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

Spread the love

 

MAMA Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania ameagiza mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato ya Serikali, kufumuliwa mara moja, ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumapili tarehe 28 Machi 2021, katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, baada ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Rais Samia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Charles Kichere, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo na mamlaka nyingine, kufanyia kazi agizo hilo.

“Naomba nizungumzie kuhusu mifumo ya malipo naomba Takukuru na CAG hebu kaeni angalieni, na pengine kuangalia hii mifumo inawezekana ikawa kazi ngumu kwenu. Angalieni, kama hamuwezi tuombe wataalamu kuangalia. Hili sio la kuchelewesha,” ameagiza Rais Samia.

Kiongozi huyo wa Tanzania ameshauri idadi ya mifumo hiyo kupunguzwa, ili ibaki michache itakayoweza kufanya kazi kwa ufanisi.

“Ndani ya Serikali kuna mifumo zaidi ya sita inayotumika kukusanya mapato, angalieni hiyo mifumo namna gani inatumika na ukusanyaji wake ukoje, mifumo ikiwa mingi tunatoa mianya ya kupoteza mapato.

Hatuna mifumo inayofanana, angalieni mifumo iwe harmonize (unganisha) tujue mifumo gani. Kama ni mitatu, mitatu. Naomba mkalisimamie hilo,” ameagiza Rais Samia.

Awali, CAG kichere wakati anatoa muhtasari wa ripoti hiyo, amesema ukaguzi wake umebaini dosari katika mifumo ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (Tehama), hasa kwenye mifumo ya ukusanyaji mapato, ambazo zinasababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

“Katika mifumo ya Tehama nimekagua, tuna ripoti tumegundua mifumo mbaimbali inajirudia, haiongee. Kuna mifumo mingine security (ulinzi) yake sio nzuri, kuna mianya kadha inayoweza sababisha upotevu wa fedha katika kutumia hiyo mifumo,” amesema CAG Kichere.

Kufuatia dosari hizo, CAG Kichere ameishauri Serikali kuipitia upya mifumo hiyo, ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

“Ni vyema Serikali ikaangalia tupate udhibiti ili kuhakikisha mapato yanayokusanywa kweli yanaingia serikalini na hakuna ufujaji wa mapato, tunakusanya mapato mengi lakini inavuja kutokana na mifumo tunayotumia,” ameshauri CAG Kichere.

error: Content is protected !!