May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Miaka mitano ya mateso kijiji cha Kongo

Spread the love

 

NI vuta nikuvute kwa miaka mitano sasa, kati ya wakazi wa Kijiji cha Kongo, Kata ya Yombo wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani na ‘mwekezaji’ Faisal Edha Awadh.  Anaandika Hamis Mguta, Bagamoyo… (endelea).

Hekaheka hizo zinahusu matumizi ya eneo la Bonde la Mto Ruvu linalopendwa kutumiwa na wakazi wa maeneo hayo kwa ajili ya kilimo.

Faisal amekuwa aakipambana kuendelea kutumia eneo hilo hata kwa kutumia Jeshi la Polis, wananchi nao wanapambana kuhakikisha kile walichoita haki yao ya kulima kwenye eneo hilo, inaendelea.

Wananchi wanamuhumu Faisal kuvamia sehemu ya sehemu ya bonde hilo na kulitumia kwa shughuli zake, huku akitumia polisi kukamata wakulima wadogo, kuharibu mazao yao na kuchoma vibanda wanavyotumia kwenye shughuli zao za kilimo.

Baadhi ya wananchi waishio katika kijiji hicho ambao hutumia sehemu ya Bonde la Mto Ruvu kwa kilimo, wanamtuhumu Faisal, kujimilikisha eneo hilo kinyume cha sheria.

Wamedai, Faisal amekuwa akivamia maeneo yao ya asili, kuchoma moto na kufyeka mazao yao; kuingiza mifugo yake na kuwabambikizia kesi za jinai mahakamani.

Hata hivyo, Faisal anadai kumiliki eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 1,557 baada ya kulinunua mwaka 2014.

Amesema, wananchi wanaomtuhumu kuwanyanyasa, ndio waliovamia eneo lake. Anawataja anaowaita ‘wahuni watatu’ kwamba ndio wanaojifanya wajuaji.

Anasema, “hakuna mwingine zaidi ya hao watatu. Mfuate mwenyekiti wa kijiji atakuambia, mfuate mkuu wa wilaya atakuambia, mfuate OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) atakuambia.

“Mimi ndio nimevamiwa na nimenyang’anywa hekari takribani 261 za shamba langu. Mipaka yangu imehakikiwa na serikali na hao wanaonituhumu, ndio walionekana kuingia kwenye shamba langu.

“Hawa wahuni wameua ng’ombe zangu kwa kuwatumbukiza mtoni, wamejeruhi wafanyakazi wangu sita wa shambani. Niliwahi kuwapeleka polisi na kuwafunga gerezani kwa kosa hilo la kuvamia shamba,” amesema.

Suleiman Hongo, mwenyekiti wa kijiji hicho amesema, Faisal ndiye mmiliki halali wa shamba hilo akisisotiza “wanakijiji waliazimishwa maeneo hayo kwa muda, ili kulitumia kwa ajili ya kilimo.”

Nini chanzo cha mgogoro huu? 

Kwanza, shamba ambalo Faisal anadai kulimiliki, lilikuwa mali ya Kampuni ya Mzizima Farms Limited. Kampuni hiyo ilianza kumiliki eneo hilo tarehe 1 Julai 1989. Faisal amenunua shamba hilo lenye hati Na. 494 mwaka 2014, kutoka kwa Dar Bayview Properties (T) Limited.

Nayo Dar Bayview Properties (T) Limited ilinunua shamba hilo mwaka 2007 kutoka Mzizima Farms.

Hata hivyo, Faisal anasema kuwa, shamba analomiliki lina ukubwa wa hekta 1,557.0663, nyaraka zilizopo zinaonesha kuwa shamba  ambalo Mzizima Farms ilikuwa inalimiki na kisha kuliuza kwa Bayview Properties (T) Limited na baadaye kuuziwa Faisal, ukubwa wake, ni hekta 557.0663 sawa na ekari 1,376.54.

Barua ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu kwenda kwa Mkuu wa Wilaya hiyo inasema,  “tofauti na madai yanayotolewa na muwekezaji na wapambe wake, shamba hilo, lina ukubwa wa hekta 557.0663.”

Anaongeza “ni vema ikafahamika kuwa shamba lenye hati Na. 494 lililokuwa likimilikiwa na kampuni ya Mzizima Farms na mbalo tulilifufua, lina hekta 557.0663 sawa na ekari 1,376.54 na sio hekta 1,557.0663.”

Barua ya mkurugenzi wa halamshauri ya Bagamoyo, kwenda kwa mkuu wa wilaya, iliandikwa tarehe 18 Januari 2019. Ilibeba kichwa cha maneno kisemacho: “Taarifa ya ufufuaji wa shamba Na. 494 mali ya Mzizima Farms, lililopo kijiji cha Kongo, Bagamoyo.”

Katika barua hiyo, yenye Kumb. Na. BAG/4130/5, Mkurugenzi Mtendaji wa Bagamoyo anasema, baadhi ya mawe yaliyokuwa yamepandwa kwenye mipaka ya asili ya shamba hilo, yalihamishwa kutoka katika maeneo yake.

Hata hivyo, mpaka sasa, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuzuia muwekezaji kunyanyasa raia na kuwanyima haki yao ya kijipatia kipato, kinachotokana na jasho lao.

Akizungumzia mipaka halisi ya shamba hilo, mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo anasema, “hata tulipokokotoa zaidi, tulipata ukubwa wa shamba hili, kuwa ni hekta 557.066 na siyo 1,557.066 zilizokuwa zinadaiwa na Faisal.

“Kazi hii, haikuwa nyepesi kwa kuwa “baadhi ya mawe yalionekana kuwa ya shamba lingine Na. 495 lililopo Chasimba,” inaeleza taarifa ya mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kitendo cha kuhamisha mawe kutoka mipaka yake ya asili, ndiyo kiini cha mgogoro unaofukuta.

Ni kitendo hicho, kilichosababisha eneo lote la bonde la mto Ruvu, ambalo wanakijiji walikuwa wanalitumia kwa kilimo, lionekane ni sehemu ya shamba la Faisal.

Kuna hata maelekezo kutoka kwa afisa wa Ardhi wa wilaya ya Bagamoyo, aliyeagiza yafanyike marekebisho ili shamba hilo, libaki na hekari zake 557.0663 zinazotambulika kisheria.

Hatua hiyo, imeifanya hati hiyo sasa, kusomeka kuwa shamba lina ukubwa wa hekta 1,557.0663, badala ya 557.663 zinatambulika kisheria.

Mara kadhaa, kumeripotiwa taarifa za baadhi ya wananchi wa maeneo hayo kukamatwa na polisi, kuwekwa rumande, kushitakiwa mahakamani na wengine hata kufungwa.

Wengi wao, wamekuwa wakituhumiwa kuingilia eneo la muwekezaji wakati nyaraka zilizotolewa na serikali, zinaonesha eneo linalogombaniwa, siyo mali halali ya Faisal.

Miraji Bigo, aliyeishi katika kijiji hicho tangu mwaka 1974, anadai kuwa muwekezaji huyo ananyanyasa raia na kuongeza, kuna siku alilazimika kutoroka nyumbani kwake usiku wa manane na kumuacha mkewe, ili kujinusuru na polisi waliokuwa wanamtafuta.

Alikuwa akituhumiwa kuingilia eneo la muwekezaji, kujeruhi mifugo yake na kuwavamia wafanyakazi wake.

“Tunamsikia Rais (John Magufuli), anavyokaripia watumishi wa umma kwenye mikoa mingine. Tunamsikia Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), anavyokemea huko kwingine. Tunamsikia Waziri wa Ardhi (William Lukuvi), lakini hapa hatujajua tupo kwenye nchi gani.

“Serikali ya kijiji tunayo, lakini hatuiamini, kwa kuwa imewekwa mfukoni na muwekezaji. Jeshi la Polisi tunalo, lakini badala ya kulinda usalama wa raia na mali zake, linamlinda muwekezaji aharibu mali za raia,” amesema.

Mwajuma Mkawa, ambaye wazazi wake, ni miongoni mwa walioanzisha kijiji hicho, anaeleza kuwa mashamba hayo, yalianzishwa na aliyekuwa rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere. Ilikuwa kipindi cha “Operesheni Pwani.”

Anasema, wakati huo, ilikuwa ni msitu na wao wenyewe ndio waliovunja pori, na kwamba wameishi katika eneo hilo kwa muda wote, bila kubughudhiwa.

Anasema, “sisi hatuna nguvu tena, tunategemea watoto wetu ambao wamekuwa wakubwa. Lakini hawawezi kwenda kule bondeni, wanakamatwa na kufungwa. Hata mimi mwenyewe, pamoja na uzee wangu, nimeshawekwa ndani. Inasikitisha sana, naambiwa amekuja mwarabu na kudai hili eneo lake. Najiuliza ametoka wapi?” amesema.

Pia Faisal amekuwa akituhumiwa kutumia polisi kukamata wananchi waishio katika kijiji hicho, kisha kuwafungulia kesi za jinai mahakamani kwa madai ya kuvamia eneo lake.

Imeelezwa, tarehe 9 Oktoba mwaka 2020, polisi kutoka Kituo Kikuu cha Bagamoyo, walifika eneo hilo na kuchoma moto vibanda na kuteketeza bamia zilizokuwa shambani na zile zilizokuwa zimevunwa.

Pia baadhi ya wananchi walifunguliwa mashitaka- Hamis Fungo na Mohamed Kifua – ambapo walidaiwa kuingia katika eneo la muwekezaji kinyume cha sheria.

Katika shauri hili la jinai, Fungo na Kifua, walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani.

Lakini hukumu hiyo ya mahakama ya wilaya, ilifutwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, chini ya Jaji Wilfred Dyansobela, na kuamuru watuhumiwa wote wawili kuachiwa huru.

Kabla ya Jaji Dyansobela, kufikia maamuzi hayo, Jaji Augustine Shangwa, alikuwa amewapatia waomba rufaa hao wawili – Fungo na Kifua, dhamana wakati wakisubiri usikilizwaji wa rufaa yao.

Jaji Dyansobela, hakuishia kuwachia huru watuhumiwa, bali alimuekeleza muwekezaji, kama anaona eneo hilo ni mali yake, afungue kesi mahakama ya ardhi. Akaonya kuwa kitendo cha kujificha kwenye jinai, wakati kesi inahusu migogoro ya madai ya ardhi, siyo sahihi.

Wakati hayo yote yakiendelea, Fungo na Kifua, wakafunguliwa kesi nyingine mbili mahakamani: Kumpiga mapanga meneja wa shamba la muwekezaji; na kuvunja ukuta na kuiba ng’ombe 45 wenye thamani ya Sh. 155 milioni.

Safari hii, Mahakama ya Bagamoyo ilieleza bayana kuwa kesi hizo zinahusu mgogoro wa ardhi, hivyo zinapaswa kupelekwa kwenye mahakama ya ardhi na siyo mahakama za jinai.

Fungo na Kifua, wamefunguliwa tena mashitaka mengine mawili mapya katika Mahakama ya Bagamoyo. Wanatuhumiwa kuingia kwenye shamba bila idhini ya mmiliki na kuchoma majani kwenye shamba lenye ukubwa wa hekali 20, yenye thamani ya Sh. 6 milioni.

Fungo na Kifua, wamekuwa wakifunguliwa kesi hizo mfululizo, kutokana na uamuzi wao wa kuendelea kulitumia eneo hilo kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga.

Rajabu Shemndolwa, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bagamoyo alipoulizwa kuhusu tuhuma kuwa jeshi lake linatumiwa na muwekezaji kukandamiza wananchi, haraka alisema, “siwezi kuzungumza lolote kuhusu jambo hilo, kwa kuwa mimi siyo msemaji wa Jeshi la Polisi.”

Alipotakiwa kueleza kama angalau anafahamu kuwapo kwa mgogoro huo, Shemndolwa bado aling’ang’ania kuwa “mimi siyo msemaji.”

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa Pwani, Wankyo Nyingesa alisema, hana taarifa za madai ya wananchi kulituhumu jeshi la polisi kutumiwa na muwekezaji.

Amesema, Polisi huwa hatumiki. Polisi huwa tunaitwa kwenye tukio; hii ni taasisi kubwa inaheshimika, hatuna taarifa zozote za muwekezaji kufanya chochote.”

error: Content is protected !!