Monday , 30 January 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Miaka 60 ya Uhuru, Zitto Kabwe ataja mambo manne kurejesha umoja
Habari za SiasaTangulizi

Miaka 60 ya Uhuru, Zitto Kabwe ataja mambo manne kurejesha umoja

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo
Spread the love

 

WAKATI Tanzania Bara ikiadhimisha miaka 60 ya Uhuru, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameishauri Serikali kutekeleza mambo manne muhimu ili kurudisha umoja ndani ya Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Zitto ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Disemba, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kutafakari masuala machache kuhusu Tanzania.

Ametaja mambo hayo kuwa kwanza; yafanyike mazungumzo ya viongozi wa vyama vya siasa ili kutafakari na kurekebisha makosa makubwa ya 2019 na 2020.

“Kwamba kiongozi mwenzetu wa kisiasa, ndugu Freeman Mbowe aliyepo jela makosa yake ni ya kisiasa na suluhisho lake lazima liwe la kisiasa sio la kijinai.

“Nazisihi Mamlaka zinazohusika na mashtaka kuwa ndugu Mbowe aachiwe Huru ili tuwe naye kwenye mazungumzo kati ya Rais na vyama vya siasa mnamo tarehe 16 – 17 Disemba 2021,” amesema.

Pia amesema mazungumzo ya vyama vya siasa yajikite kwenye kuangalia namna nzuri ya kuandika upya Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya siasa. Vile vile Sheria mbalimbali kandamizi zitazamwe upya na kurejewa.

“Mwaka 2022 tunatimiza Miaka 30 tangu Nchi yetu irejee kwenye mfumo wa vyama vingi vya Siasa. Ni muhimu sasa kuanza majadiliano na mazungumzo rasmi kitaifa kuhusu namna ya kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya,” amesema.

Amesema angetamani miaka 60 ijayo, Taifa liendelee kuwa moja, lenye ushawishi kwenye ukanda huu na duniani kwa ujumla.

“Taifa lenye wananchi wanaojitambua, wenye maarifa, wasio masikini na wanaopendana. Bila Kuwa wamoja sasa hatutaweza kukaa pamoja na kujenga hilo ninalotamani kurithisha kwa vizazi vinavyokuja. Lakini ili kuwa wamoja ni lazima kuimarisha mifumo ya Haki ili kudumisha Amani. Tusiogope kujadiliana,” amesema.

Amesema mambo hayo yanatakiwa kufanyika haraka ili Taifa lina miaka 60 ya Uhuru lakini bado hakuna uhuru na ustaarabu wa kuchagua viongozi kwa haki.

“Tukiitisha uchaguzi ni lazima tuuane; Tuna miaka 60 lakini hatuvumiliani kisiasa, tunashutumiana na hata kufungana, tunazuiana kufanya shughuli halali za kisiasa, tuna miaka 60 lakini bado tu masikini,” amesema.

Amesema ni vigumu kuendelea namna hiyo huku Taifa likitarajia kuwa mambo yatabadilika yenyewe.

Amesisitiza ni muhimu sana kufanya tafakari ya pamoja kama Taifa ili kujenga matumaini ya Taifa letu kutupeleka miaka 60 ijayo.

“Ninachokishauri si kipya, alikishauri mzee wetu, Rais wa Awamu ya Nne, ndugu Jakaya Kikwete wakati tulipoadhimisha miaka 50 ya Uhuru, kwamba ni furaha kuwa Taifa letu kutimiza miaka 50, lakini ni muhimu tujitafakari na kuja na njia mpya ya kuendea miaka 50 inayofuata, njia ya mzee Jakaya ilikuwa ni kuanzisha “Mchakato wa Katiba Mpya”.

“Tulitumia miaka mitatu kujadiliana kama Taifa juu ya Katiba yetu mpya iweje, ingawa mchakato ule hatukuumaliza lakini yapo mafunzo ambayo tumeyapitia kama Taifa, kwanza kwa kutoumaliza ule mchakato, na pili kwa kuuona umuhimu wa ule mchakato.

“Matokeo ya maono ya Watanzania kwa miaka 50 inayokuja yaliwekwa katika Rasimu ya Katiba na hatimaye kwenye Katiba pendekezwa.

“Sio kila mtu aliyapenda yote yaliyokuwamo katika nyaraka hizi. Hilo haliwezekani kwani wakati wowote ule nchi yetu angalau 40% ya watu wake hupingana na 60% ya watu wengine. Muhimu ni kupata mwafaka kwa kutilia umuhimu yale tunayokubaliana.

“Hatukupata muafaka wakati ule. Tukapita kwenye kipindi kigumu ambacho kinapaswa kuwa funzo kubwa ili tusirejee huko. Ni lazima turidhiane. Ni lazima tujenge Taifa ambalo kila Mwananchi anashiriki katika masuala ya nchi bila ubaguzi,” amesema.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chongolo asikitishwa na mradi wa Mil 900 kutoanza kutoa manufaa

Spread the loveKATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa matokeo ya mtihani kidato cha nne 2022

Spread the loveBARAZA la Mitihani la Tanzania (Necta) leo Jumapili limetangaza matokeo...

Habari za Siasa

NCCR-mageuzi yawaangukia Polisi kupotea kwa kada wake

Spread the loveJESHI la Polisi nchini limeombwa kufanya uchunguzi wa kina utakaosaidia...

HabariTangulizi

Bakwata wamkangaa Sheikh wa Dar es Salaam

Spread the love  BARAZA la Ulamaa, limefutilia mbali uamuzi wa “kuvunja ndoa,”...

error: Content is protected !!