September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Miaka 45 ya CCM: Chongolo atoa maagizo kwa wenyeviti

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

Spread the love

 

KATIBU Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amewaagiza wenyeviti wa CCM mkoa na wilaya kutenga siku maalum kwa wanachama na wananchi kushiriki matembezi ya mshikamano kwa lengo la kuhamasisha shughuli za maendeleo na kuimarisha afya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).

Chongolo ametoa agizo hilo leo asubuhi Jumamosi, tarehe 5 Februari 2022 wakati alipomuwakilisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, katika matembezi ya mshikamano ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 45 tangu kuzaliwa kwa CCM.

Maadhimisho hayo kitaifa yanafanyikia Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara na mgeni rasmi ni Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samian a wageni mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete.

Amesema fedha zilizopatikana katika matembezi ya mshikamano ya kuzaliwa kwa CCM, zitaelekezwa katika shughuli ya uchapaji kadi za kieletroniki kwa wanachama.

“Matembezi haya ni chagizo kuu la maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM katika kipindi chote. Baada ya hapa ninategemea wenyeviti wa CCM mkoa na wilaya watatenga siku maalum ya matembezi,”amesema.

Chongolo amesema dhumuni la matembezi hayo ni kukifanya chama kuendelea kujitegemea kwa kutunisha mfuko wa uendeshaji shughuli za CCM.

Amesema dhumuni la kufanya hivyo ni kuwa na muda wa kufanya mazoezi na kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo huko ndiko kuenzi uasisi wa matembezi ya mshikamano.”

“Ndio maana mwaka huu tumetoa fomu kwa lengo la kukusanya fedha za kutunisha shughuli za uendeshaji chama na fedha zote zitakazipatikana zinaelekezwa kwenye uchapaji kadi za kieletroniki,” alisisitiza, Chongolo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara, Chiristina Mndeme, amesema Ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa kwa vitendo, hivyo wananchi waendelee kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Mabodi, amesema wana CCM kuendelea kudumisha umoja na mshikamano na kuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za maendeleo.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia amedhamiria kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata maendeleo kupitia sekta mbalimbali.

“Rais Samia anendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa vitendo na tunaamini atatuvusha kufikia lengo la kila mwananchi kunufaika kupitia maendeleo yanayopatikana nchini,” amesema

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Mzengo Pinda, amesema tangu kuzaliwa kwa CCM taifa limeendelea kuwa lenye amani na mshikamano.

“Katika miaka yote 45 tangu kuzaliwa kwa CCM ajenda kuu ilikuwa ni maendeleo kwa wananchi, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuendeleza moyo wa uzalendo, amani na mshikamano ili maendeleo zaidi yapatikane,” amesema.

error: Content is protected !!