January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Miaka 16 gerezani imenipatia ujuzi

Donald Nyondo, akiwa kazini kwake.

Spread the love

“Tuliteka gari na kuliiba. Baada ya tukio hilo tukiwa mjini tukakamatwa na kufikishwa polisi na baadaye kupelekwa mahakamani, tukikabiliwa na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Maisha yangu yalikuwa ya wizi na unyang’anyi mpaka nilipokamatwa katika tukio hilo. Tamaa ya kupata maisha mazuri haraka ndiyo iliniponza. Lakini sasa najuta kwani nilipoteza muda wangu”

Hii ni kauli ya Donald Nyondo (39) mkazi wa jijini Mbeya ambaye ni mzaliwa wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea katika kiwanda chake cha usaremala.

Nyondo anasema “nilihukumiwa 14 Aprili 1999, kutumikia kifungo cha miaka 45 jela baada ya kutiwa hatiani na Mahakama katika kesi iliyokuwa ikinikabili ya unyang’anyi wa kutumia silaha.”

Anasema baada ya hukumu hiyo kutolewa, hakuridhika nayo na hivyo mwaka 2000, aliamua kukata rufaa katika Mahakama Kuu lakini huko akapigwa mweleka.

“Niliamua kwenda Mahakama ya Rufaa ambako baada ya miaka mingi kupita, Juni 2014, niliachiwa huru baada ya kukaa gerezani miaka 16 nikiwa nimepitia katika magereza tofauti ya Songea, Ukonga, Ruanda na Iringa.

“Nilipoanza kutumikia kifungo, awali maisha yalikuwa magumu. Niliona kama ni mwisho wa maisha yangu na nikakata tamaa kabisa. Lakini kutokana na ushauri wa askari magereza na wafungwa wenzangu kwamba, kifungo sio mwaisho wa maisha, nilipata faraja nikatulia,” anasema Nyondo.

Jeshi la Magereza kupitia miradi yake mbalimbali, linatekeleza programu ya urekebishaji wafungwa kwa kuwapatia ujuzi tofauti ili wamalizapo vifungo vyao waweze kujitegemea badala ya kurejea uhalifu.

Nyondo ni mmoja wa matunda ya progaramu hiyo. Sasa ni mjasiliamali akiwa amejiajiri katika kiwanda chake cha useremala alichokianzisha baada ya kutoka kifungoni.

“Nikiwa gerezani Ukonga nilijifunza ufundi seremala na baada ya miaka mitatu niliweza kumudu kutengeneza vitu mbalimbali kwa umahiri mkubwa na hapo ikawa mwanzo wa maisha yangu mapya, kwani nilianza kufanya kazi vizuri na utii nikiamini nimepata fani ambayo itakuwa mkombozi wa maisha baada ya kifungo,” anasema.

Nyondo ambaye amezaliwa katika kijiji cha Kibao, Mufindi mwaka 1975 akiwa mtoto wa tano katika familia ya watoto saba, alisoma shule ya msingi Ipilima na kumaliza darasa la saba.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi, hakutaka kuendelea na masomo, akajiunga na makundi mabaya ambayo kazi yake ilikuwa kuiba wakizunguka katika mikoa tofauti akiwa na miaka 23.

Nyondo anatamba kuwa “Siwezi kukubali kuajiriwa na mtu kwa sasa kutokana na uwezo wangu kuwa mkubwa sana katika kazi ninayoifanya. Samani ninazozitengeneza hapa kiwandani naamini siku moja zitafika mbali.”

Anafafanua kuwa, kwa kushirikiana na wenzake kiwandani hapo, wanatengeneza meza, sofa, viti, vitanda, kabati na vitu vingine kulingana na oda ya mteja.

“Kutokana na ubora wa samani zetu, wakati mwingine hata Magereza wakiwa na oda nyingi za wateja wao, wananiletea hapa kwa sababu wanatambua uwezo wangu,” anasema.

Nyondo mwenye familia ya mke mmoja na watoto wawili, anasema siri ya mafanikio yake ni kauli nzuri, uaminifu katika kazi kwa wateja wake na umahiri wa kutengeneza samani.

Anaongeza kuwa, “nikipima maisha yangu kabla na baada kifungo, najiona kama tuko watu wawili tofauti kwa sababu naona mabadiliko makubwa sana yaliyopo katika maisha yangu sasa.”

“Namshukuru Mungu, lakini pia Jeshi la Magereza kwa kiasi kikubwa limeweza kunijenga na kunifanya niwe hivi nilivyo leo. Nimekuwa mtu ninayejitambua,” anasema.

Akimzungumzia mfungwa huyo wa zamani, Mkuu wa kiwanda cha Ruanda cha Gereza kuu la Mbeya, Mrakibu Mwandamizi, Huruma Mwaliaje anasema “Nyondo ni kijana mwenye mfano mzuri kwa jeshi la magereza. Amejitahidi kutumia mafunzo aliyopata gerezani na sasa amejiajiri.”

Mwaliaje anafafanua kuwa “Kijana huyu nimekaa naye mwaka 1999 akiwa Gereza la Ukonga, baadaye tulikutana hapa Ruanda akiendelea kutumikia adhabu yake. Ni kweli alikuwa msaada mkubwa sana katika kiwanda chetu kutokana na bidii yake ambayo leo imempa mafanikio haya ya kuwa na kiwanda chake.”

Kwa mujibu wa Mwaliaje, Nyondo alipotoka gerezani alimuaga na kumueleza kwamba hataondoka Mbeya. Anasema aliahidi kutafuta sehemu ya kufanyia ufundi wake, jambo ambalo waliliafiki na kumshauri atafute eneo la karibu na gereza ili waweze kumsaidia atakapokwama.

error: Content is protected !!