July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mhariri MwanaHALISI Online afariki dunia

Marehemu Edson Kamukara enzi wa uhai wake akiwa kazini

Spread the love

MHARIRI mwanzilishi wa gazeti la hili, Edson Kamukara, amefariki dunia leo Alhamisi, majira ya saa 12 jioni, nyumbani kwake, Mabibo jijini Dar es Salaam. 

Msiba wa marehemu Kamukara uko nyumbani kwa dada yake Makongo Juu, jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Katika maisha yake ya uandishi wa habari, Kamukara alifanya kazi katika vyombo vingi kikiwamo gazeti la Majira, Jambo Leo na Tanzania Daima. Alijiunga na MwanaHALISI ONLINE, Februari mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, MSETO, MwanaHALISI ONLINE na mtandao wa MwanaHALISI Forum, Saed Kubenea amethibitisha kifo cha mwandishi huyo na kusema:

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuondokewa na mwenzetu Kamukara ambaye tulimfahamu na kumpenda.

Nilianza kufahamiana na Kamukara wakati akiwa gazeti la Tanzania Daima. Namfahamu kama mchapakazi, mwadilifu na mkweli. Alikuwa anashindana kwa hoja.

Yeye ndiye alikuwa mhariri wa kwanza wa gazeti hili. Niliongea naye kwa simu mara ya mwisho Jumapili iliyopita, wakati akiwa nyumbani kwao Bukoba, mimi nikiwa njiani naelekea Dodoma. 

Ni katika mazungumzo yetu hayo, ndipo aliponieleza kuwa alikuwa anasumbuliwa na malaria. 

Ni mmoja wa waandishi wachache nchini walioamini kwamba maadili ya uandishi hayatungwi na serikali wala wanasiasa wenye uchoyo wa kuandikwa kwa mapambo, bali wanataaluma wenyewe.

Tulizungumza mengi kuhusu kazi, lakini nikamtaka ajipumzishe zaidi na kuhakikisha kuwa anapata matibabu ya kutosha.

Nilikuwa nampigia simu usiku wa manane Kamukara kumweleza kuhusu habari ambayo tulipaswa kuijadili, kesho yake alifika ofisini saa moja asubuhi.

Kwa kweli, alikuwa na bidii sana na kazi. Alikuwa tegemeo kwa kampuni na pengo alilotuachia, ni vigumu kuliziba.”

Kubenea anasema, mpaka sasa, haijajulikana wazi, sababu ya kifo cha mwandishi na mhariri wake, ingawa anachofahamu ni kuwa alikuwa anasumbuliwa na malaria.

Anasema, Kamukara alirejea jijini Dar es Salaam leo asubuhi kutokea Bukoba, ambako alikwenda kumjulia hali mama yake mzazi ambaye ni mgonjwa.

Taarifa zinawanukuu majirani wakisema, Kamukara alijisikia vibaya wakati anaenda dukani kununua dawa, ghafla alianguka ambapo majirani walimsaidia kumpepea na baade kumpeleka kwake ambako alipumzika hadi alipopata nguvu.

Hata hivyo, ghafla majirani walianza kusikia kishindo ndani ya nyumba hiyo na baada ya kuingia ndani, walimkuta akiwa ameanguka, huku fulana aliyokuwa amevaa ikiwa imeungua moto na yeye kutoka damu nzito iliyotapakaa kwenye sakafu.

Aidha, televisheni ilikuwa imepasuka, pamoja na vifaa vingine vidogo vidogo vya ndani navyo vilikutwa vimepasuka, jambo ambalo linaonyesha kama kulikuwa na purukushani au alikuwa akivunja vitu hivyo.

Tutaendelea kuwapa habari zaidi.

error: Content is protected !!