September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mhadhiri UDSM ajitosa ubunge Segerea

Spread the love

MHADHIRI wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse amechukua fomu kuwania ubunge jimbo la Segerea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

Dk. Jesse amechukua fomu hizo leo Jumanne tarehe 14 Julai 2020 katika ofisi ya chama hicho Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Bonnah Kamoli ni mbunge anayemaliza muda wake kupitia CCM ambaye ameongoza kwa muhula mmoja wa miaka mitano.

Amesema baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kama mtumishi wa umma sasa ameona ni wakati muafaka wa kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendekeo kwa njia nyingine.

“Chama kinataka watu watakaoweza kuwaletea wananchi maendeleo na mimi nimejitafakari nimeona uwezo huo ninao kama chama kitanipa ridhaa,” amesema Dk. Jesse.

Msomi huyo ambaye alikuwa askari wa Jeshi la Polisi kwa miaka 10 alimpongeza Rais John Magufuli kwa kusimamia vyema rushwa kwa maelezo kuwa utaratibu unaotumika sasa CCM umepunguza vurugu hasa mitaani.

“Chama kimeandaa utaratibu mzuri kwa wagombea utakaosaidia kupunguza vurugu kwenye majimbo mgombea akishachukua fomu anajaza na kuirejesha kisha anasubiri siku ya uteuzi, ni jambo zuri kwa kweli,” alisisitiza.

Dk Jesse (49)  ni mhadhiri wa sheria UDSM na kwa sasa anaongoza Idara ya Sheria Binafsi ambayo ni moja kati ya Idara Kuu  tatu za Shule Kuu ya Sheria ya UDSM.

Kuhusu kujiunga kwake na Jeshi la Polisi licha ya  kufaulu alama za juu kidato cha sita na kuchaguliwa kujiunga na UDSM amesema, “nilikuwa nikifurahishwa  sana kila alipokutana na Polisi njiani. Mavazi yao na jinsi walivyokuwa waking’arisha viatu vyao yalinifurahisha.  Kujiunga polisi niliona nimetimiza ndoto.”

Ameema alipangiwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wakati akilitumikia jeshi hilo aliendelea na masomo UDSM mpaka alipoacha na kujikita katika taaluma yake ya sheria mpaka kuwa mhadhiri wa chuo hicho.

“Nina shahada nne katika sheria. Niliamua kusoma kwa sababu mtu yeyote akiwa UDSM kama mhadhiri anapaswa kuwa na uelewa mpana sana wa mambo. Kwahiyo kadri anavyosoma ndivyo anarutubisha ubongo wake,” amesema.

error: Content is protected !!