Klabu ya Soka ya Simba imemtangaza Juma Mgunda kuwa kocha wa muda wa klabu hiyo atakayesaidiana na Seleman Matola, kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Nyassa Big Bullet ya nchini Malawi. Anaripoti Mwandishi Wetu.
Mchezo huo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa utapigwa tarehe 10 Septemba 2022, ambapo Mgunda atakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachosafiri hapo baadae kuelekea nchini Malawi.
Taarifa ya klabu ya Simba ilitolewa usiku wa jana septemba 7 mwaka huu, muda mchache mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Kmc imekeza kuwa, Mgunda ni kocha mwenye leseni A ya Shirikisho la soka barani Afrika (CAF), na hivyo kukidhi vigezo vya kuiongoza timu hiyo.
Simba imeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia hivi karibuni kuachana na kocha wake Zoran Maki ambaye amedumu katika kipindi cha miezi mitatu ndani ya klabu hiyo.
Kikosi hiko kinakwenda kwenye mchezo huo, huku kikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Kmc uliopigwa siku ya jana kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, Mgunda atakuwa na kikosi hiko mpaka pale mchakato wa kumpata kocha mkuu utakapo kamilika.
Leave a comment