January 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgongano wa maslahi ni pango la CCM

Rais Jakaya Kikwete

Image 3

Spread the love

MAKABURI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni mengi sana. Mojawapo ni utamaduni wa kuendesha serikali kwa kupuuza migongano ya maslahi kati ya watendaji na serikali yao, au kati ya watendaji wa chama na serikali; na ama wananchi waliowachagua.

Wakati wa mjadala wa wizi wa fedha za umma kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Rais Jakaya Kikwete alisikika akisema, unaandaliwa utaratibu wa kutenganisha shughuli za biashara na kisiasa miongoni mwa wanasiasa na watendaji.

Muda mfupi baadaye niliwasikia baadhi ya wabunge ambao ni wafanyabiashara wakitishia kuwa akithubutu kufanya hivyo, wataunda chama cha siasa cha wafanyabiashara na kuking’oa CCM madarakani.

Tangu wakati huo, sijamsikia tena rasi wetu akikumbusha azma yake hiyo na wala sijamsikia mtendaji yeyote wa chama akizungumzia suala hili, ukiacha kelele za hapa na pale zinazopigwa na makada wastaafu au wale walioumizwa na rafu za fedha za wafanyabiashara.

Kimya cha rais au kusita kutekeleza azama yake hiyo, ni kaburi kwa chama chake. Mgongano wa maslahi katika maisha ya kisiasa na kiserikali katika nchi hii, ni uwanja ambao hauwezi kuzibwa na sheria iliyopo sasa.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliliona hili mapema. Akaamua kuziba mianya inayoachwa na sheria iliyopo kwa kuunda miiko ya uongozi. Aliwabana watendaji wa serikali waliojihusisha na vitendo vyenye mwelekeo wa mgongano wa maslahi.

Kiongozi wa serikali au wa kuchaguliwa akifanya biashara na serikali, ni mgongano wa maslahi. Hili ndilo eneo kuu linalozungumzwa sana na kulalamikiwa. Lakini ni moja tu. Watendaji wengi baada ya kubaini kelele katika eneo hili, hutumia mkono wa pili au hata wa tatu kufanya biashara na serikali.

Mathalani, mtendaji aweza kusajiri kampuni kwa jina jingine au hata kununua hisa nyingi kwa kutumia jina jingine katika kampuni ambayo baadaye yeye au watendaji wenzake wanaipa tenda ya kufanya biashara na serikali.

Biashara hii yaweza kuwa katika ofisi ya mtendaji huyo, lakini ili kuzuia kelele na kukwepa mkono wa wenye fitina, anaweza kuzungumza na watendaji wa aina yake katika mikoa ya mbali ili kukamilisha azma hiyo.

Ushahidi wa tabia hii unaonekana kwa njia ya ongezeko la vitendo vya utapeli au vitisho kwa watendaji waaminifu kwa kutumia majina ya wakubwa serikalini na kwenye chama tawala. Matumizi ya majina haya yana tafsiri moja kubwa, nayo ni kuwa ukiwa rafiki, jamaa au hata kumjua mtu mkubwa katika serikali na chama tawala, unakuwa na kinga ya kukamatwa au kuzuiwa kufanya unachopenda.

Mtu aweza kusafiri mwendo mrefu na kupata huduma bure popote aendapo ili mradi ataje jina la mkubwa mmoja katika vyombo vya dola, serikali au CCM. Kwa bahati mbaya, sijamsikia mkubwa yeyote akija hadharani kuwatangazia Watanzania kuwa yeyote atakayetumia jina lake asisikilizwe na akisikilizwa basi yule aliyemsikiliza achukuliwe hatua kali.

Hata inapotokea ndugu, rafiki au mbia wa mtu mkubwa amekamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola, jitihada hufanyika na mtu mkubwa huyo au wasaidizi wake kuhakikisha mtuhumiwa anapewa dhamana na hapo hapo mlolongo wa kuweka sawa jambo hilo huanza kwa kuwaona waendesha mashtaka, mawakili na hatimaye mahakimu na majaji.

Haya si mambo yanayoweza kusemwa hadharani na wahusika lakini itoshe kuwa jamii inajua mengi na kimya cha jamii hakina maana kuwa mambo ni shwari.

Hata inapotokea kwa sababu na mazingira yasiyoweza kuepukika kwamba mhusika aliye karibu na wakubwa amehukumia kifungo, kwanza mashtaka hupigwa dana dana na kupunguzwa makali na baada ya hukumu, hatua za msamaha huanza mara moja.

Haya yanaweza kufanyika kwa kumhusisha mkubwa mwenyewe au hata bila kumpa taarifa ilimradi wanaoshughulikia suala wana uhakika kuwa mwisho wa siku atajua na kuwashukuru. Huu ni mgongano wa maslahi kwa sababu serikali ile ile inamshtaki na kumhukumu mhusika, kisha serikali ile ile imamsaidia mhusika kupeuka adhabu.

Pamoja na kwamba kuna uwezekano wa serikali kufanya hivyo bila kuvunja sheria, bado ni mgongano wa maslahi kwa sababu mhalifu na mtekelezaji wa sheria wana uhusiano wa kinasaba au kirafiki.

Mtindo huu wa utawala unaoruhusu mgongano wa maslahi ni kwa pande zote mbili, yaani, pale unasaba unapotumika kuzuia sheria kufanya kazi yake au pale unasaba unapotumika kujipatia maslahi na kipato.

Tuchukulie mfano mdogo katika Ikulu yetu kama ambavyo imetazamwa tangu awamu ya pili mpaka sasa. Mke wa rais anapotumia nafasi yake kama mke wa rais kuanzisha asasi, kisha akakusanya fedha toka ndani na nje ya nchi, akazitumia fedha hizo kwa kadri ya mapenzi yake, ni mgongano mkubwa wa maslahi.

Matumizi ya nafasi na jina la rais kujipatia fedha ni sawa tu na wale matapeli wanaotumia jina la rais kuwaibia watu au hata kuwatoza rushwa. Mke wa rais anapokuwa katika msafara wa rais nje ya nchi na kutumia mwanya huo kukusanya fedha kwa ajili ya asasi yake, anakuwa amesababisha mgongano wa maslahi kwa sababu anaposafiri anatumia fedha za walipa kodi, lakini fedha anayopata huko kwa ajili ya asasi yake ni kwa manufaa yake binafsi na kisiasa.

Pamoja na kwamba wake wa marais wetu na watoto wao wana maisha binafsi na wana haki ya kufanya shughuli zao za kibiashara bila kubugudhiwa, lakini daima wakumbuke kuwa mme wao na baba yao yuko katika ikulu yetu na jina lake ni hazina kubwa ya taifa.

Hoja hii yaweza kupuuzwa kwa madai kuwa ikiwa watendaji wanawapendelea kwa kuwaogopa si kosa la mke na mtoto wa rais, bali ni la watendaji hao. Hali si nyepesi namna hiyo, kwa sababu wananchi wamewekwa madaraka makubwa mno mikononi mwa mtu mmoja aitwaye rais na kwamba kivuli cha mtu huyo kinatosha kuwatisha watendaji wanapokutana uso kwa uso na jamaa za rais huyo.

Matokeo ya mtindo huu wa muda mrefu, ni kusababisha utendaji serikalini kuwa mbaya. Uzembe na ubadhilifu wa mali ya umma unaidhoofisha serikali kwa sababu ya kulindana. Rais Kikwete amewaita watendaji wa namna hii kuwa ni michwa katika halmashauri zetu.

Haya ni maneno ya kukata tamaa na kukatisha tamaa wananchi. Makabati ya vyombo vya dola yamejaa kumbukumbu za madhambi ya wakubwa na jamaa zao. Kimsingi hakuna uwezekano chini ya utaratibu wa sasa, kwa mkubwa au jamaa yake kuhukumia kifungo, acha mbali kulala mahabusu!

Tayari taifa limeunda tabaka la watu wasioguswa na mkono wa sheria. Wanyonge hawana haki tena, jambo ambalo limefanya chuki ya wananchi dhidi ya serikali na chama tawala kuongezeka. Chama tawala kinapokuwa sehemu ya serikali, nao ni mgongano wa maslahi. Mnyororo huu hauna mwisho ni mpaka kaburini!

error: Content is protected !!