January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgomo wa Walimu wanukia

Spread the love

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT), kimeonya kuwa kitachukua hatua madhubuti ikiwa katika kipindi cha siku 30, serikali itashindwa kulipa stahiki zote za walimu nchini. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hatua hiyo inatokana na serikali kupuuza madai ya walimu yaliyotaka kulipwa madeni yao yote wanayoidai serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Rais wa CWT, Gratian Mukoba amesema, serikali imepuuza matatizo yao na kushindwa kutoa majibu yasiyoridhisha na yasiyo na utatuzi.

Amesema, awali chama chake na werikali walikubaliana kuwepo kwa muundo mpya wa utumishi kwa waalimu; muundo ambao ulipangwa kuanza kutumika mwaka wa fedha wa 2014/2015. Mfumo ulipitishwa katika mwaka 2013/2014.

Muundo huo mpya ulihusisha matatizo makubwa tisa; na ambayo serikali ilikubali kuyatekeleza.

Mukoba ameeleza miundo hiyo ambayo ilitarajiwa kutekelezwa miaka miwili iliyopita, ni pamoja na muundo mpya wa utumishi wa waalimu; posho ya madaraka kwa wakuu wa shule; upandishaji wa madaraja; madeni na muundo wa wakaguzi wakuu wa shule.

Anasema, serikali na CWT walijifunga katika makubaliano yaliyotaka waalimu zaidi ya 40,000 kupanda madaraja; kuanzia Julai mwaka huu, jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezwa.

Mukoba amesema, walimu wanaidai serikali zaidi ya Sh. 19 bilioni, huku walimu zaidi ya 38,000 waliopanda madaraja wakiwa hawajalipwa mishahara.

Matatizo mengine, ni nyongeza ndogo za mishahara na ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu ambapo amedai, kuna waalimu hawajalipwa viinua mgongo tangu mwaka 2014.

Amesema, baada ya kuyapeleka matatizo hayo serikalini hadi leo hakuna majibu ya kuridhisha kutoka kwao badala yake wanakimbia vikao na walimu.

Anasemaa, “Agosti 19 mwaka huu, tulipanga kuwa na kikao cha mwisho cha kujadili changamoto hizi. Lakini serikali imekataa kukutana nasi. Sasa tumepanga kukutana Agosti 28; kikao hiki cha sasa kitakuwa cha mwisho.”

Anasema, “…tumeshachoka kupigwa danadana na hata wakija kikaoni wanakuja na agenda tofauti.safari hii hatutaki ahadi tunaitaji vitendo.”

Anahoji: Kwa nini serikali inataka hadi ishinikizwe kufanya wajibu wake kana kwamba haijui kama walitoa waraka wa muundo mpya wa walimu?

Anasema, chama chake kitakutana baada ya tarehe ya mwisho waliyokubaliana, ikiwa serikali haitatekeleza mwatakwa yao, wataamua cha kufanya.

error: Content is protected !!