January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgomo wa madereva watikisa, Serikali yanywea

Umati wa abiria walioshindwa kusafiri baada ya mgomo wa madereva katika kituo cha mabasi cha Ubungo

Spread the love

BAADA ya kutishia kugoma nchini nzima wakapuuzwa, hatimaye madereva wametimiza ahadi yao leo. Shughuli zikamasimama saa takribani saba, wananchi wakisotea usafiri ndipo Serikali ikaibuka na kuwasikiliza. Anaandika Pendo Omary …(endelea).

Sasa serikali imekubaliana na madereva hao kwamba baadhi ya kanuni zilizopitishwa na kikosi cha usalama barabarani hazitekelezeki na hivyo imekubali kutatua kero zote za madereva ndani ya kipindi kifupi.

Uamuzi wa serikali kusalimu amri umekuja baada ya maelfu ya madereva wa mabasi ya abiria na mizigo kugoma kufanya kazi nchi nzima kuanzia asubuhi ya saa 12:00 hadi 7:15 mchana muafaka ulipopatikana.

Mgomo huo umekosesha safari za mabasi yaendayo mikoani, maroli ya mizigo na daladala na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wengi.

Pia mgomo huo umesababisha kuibuka vurugu kubwa eneo la Ubungo Mataa, baada ya baadhi ya madereva kuanza kuwashambulia madereva wa pikipiki, bajaji na magari yaliyoonekana kupakia abiria na kupita eneo hilo.

Hali hiyo imelazimu Jeshi la Polisi kuingilia kati kwa kurusha mabomu ya machozi ili kuzuia mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa dhidi ya madereva waliokiuka agizo la kugoma.

Suleiman Kova- Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alijaribu kuzungumza na maelfu ya madereva hao waliokusanyika katika stendi hiyo bila mafanikio.

Kova akalazimika kumuita Gaudensia Kabaka – Waziri wa Kazi na Ajira baada ya kutakiwa kufanya hivyo na madereva.

“Tunamtaka wenzetu waliokamatwa jana waletwe hapa kisha waziri aje atujibu sio wewe Kova, vinginevyo tunaendelea kugoma,” zilisikika sauti za madreva hao.

Majira ya saa 6:30 mchana, Kabaka aliwasili ndani ya kituo kikuu cha Ubungo akiwa ameongozana na Said Meck Sadiki -Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Dk. Shaaban Mwinjaka – Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi .

Kabaka ameamua kusalimu amri kwa niaba ya serikali. Alifanya hivyo baada ya juhudi zake za kuitetea serikali kukwama huku madereva wakishikilia msimamo wao kwa kusema “hatutaki siasa katika hili. Tunataka majibu sasa hivi. Tangu nchi hii ipate uhuru tumekuwa na madai. Leo ni mwisho wa kusubili.”

Awali alipofika eneo hilo, Kabaka aliahidi kwamba “serikali itakaa na madereva hao 18 Aprili mwaka huu, kujadili kwa kina madai yao.”

“Kwa niaba ya Wizara ya Uchukuzi hilo la kusoma nalifuta kuanzia sasa. Kuanzia kesho madereva wote wanatakiwa kuwa na mikataba ya ajira. Kwa sababu mikataba ya sasa nimegundua ni geresha. Hata madreva wakiumia kazini hawana haki,” amesema Kabaka.

Kabaka amesema “kuanzia leo mwenye basi, lori ni lazima aende ofsi ya kazi akiwa na mkataba wenye picha ya dereva na dereva husika na sio kwenda na mikataba yenye picha za watu ambao ni marehemu au wa kughushi”.

“Pia tutapitia mikataba yote na kuhakaikisha madereva wanapata haki ya matibabu, likizo, saa za kazi, kodi ya nyumba . Tarehe 18 Aprili mwaka huu, tutakutana na viongozi wenu ili kuchukua hatua zaidi katika kutekeleza madai yenu kwa hatua ya muda mrefu,” ameongeza Kabaka.

Katika kusawazisha mambo, Kova akatangaza kuwa “Tayari madereva waliokamatwa jana hawa hapa nimewaleta. Na nyinyi mnawaona. Natangaza kuanzia sasa madereva waliokamatwa wameachiliwa huru na ambao hawajaachiliwa natangaza waachiliwe kuanzia sasa.”

Akizungumzia madai ya madereva, Rashidi Swalehe – Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Madereva nchini, amesema “tuna madai sita. Tunafanya kazi bila mikataba. Kwa maana hiyo hatulipi kodi kwa serikali”.

“Madai mengine ni kukosa mishahara ambapo inapelekea kuwa vibarua kwa malipo ya Sh. 30,000 kwa siku, hatutaki kwenda kusoma kwa sababu hatuwezi kugharamia masomo na malori yasikae muda mrefu Tunduma mpakani,” amesema Swalehe.

Ameongeza kuwa kukinzana kwa ratiba inayotolewa na Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kunawavuruga.

“Polisi wanatutaka tutembea kwa spidi 80 huku Sumatra wakitaka tutembea kwa spidi 150,” amefafanua Swalehe.

Aidha, madereva hao wameahidi kuendelea na mgomo iwapo serikali haitashughulikia maadhi ya madai yao katika mkutano utakaofanyika 18 Aprili mwaka huu katika ukumbi wa ofisi za Wizara ya Kazi na Ajira.

Hali hiyo ya kadhia ya mgomo, imejitokeza takribani mikoa yote nchini na hivyo kusababisha shughuli za uzalishaji kukwama kwa muda.

error: Content is protected !!