July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea wa Chadema kufikishwa mahakamani kesho

Spread the love

MGOMBEA ubunge wa jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chadema, Benson Kigaila na wenzake 10 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Watuhumiwa hao ambao wamewekwa lumande tangu Ijumaa wanatuhumiwa kufanya maandamano bila kibali huku ikidaiwa walimshambulia askari kwa chupa ya soda.

Taarifa ya kukamatwa kwa wafuasi hao pamoja na mgombea ubunge huyo ilitolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime alipokuwa akizungumza waandishi wa habari.

Misime amesema Kigaila na wenzake kumi wanadaiwa kukamatwa kutokana na kufanya maandamano bila kibali na kuzuia watumiaji wengine wa barabara kushindwa kuendelea na shughuli zao.

Mbali na kufanya maandamano bila kibali jeshi la polisi linadai kuwa wafuasi wa Chadema walimshambulia askali polisi kwa kutumia chupa ya soda kumpiga nayo kichwani sambamba na kufanya fujo kituoni.

Misime amesema matukio hayo yalitokea jana majira ya saa 12:45 kutokea barabara ya Jamatini na kituo cha polisi baada ya mgombea ubunge wa chadema kumaliza mkutano wake wa kampeni katika eneo la stendi kuu ya Dodoma.

Misime aliwataja waliokamatwa kuwa ni Benson Kigaila mgombea ubunge Chadema, Khadija Maula, Godfrey Manyanya mwenyekiti BAVICHA mkoa wa Dodoma.

Wengine ni Stellah Masawe, Hashimu Kilaini, Alex Thomasi, Prisca Mgaza, Luckyson kweka, Aisha Urio, Pompey Remijo na Lawi Tumuza.

Kamanda amesema kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi wanaandaliwa jarada kwa ajili ya kuwapandisha kizimbani siku ya kesho.

Kutokana na hali hiyo kamanda Misime amesema kuwa jeshi litaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua wanasiasa ambao watafanya kampeni zao ambazo ni za kuvunja amani.

Hata hivyo Misime hakuweza kumtaja jina askari aliyedaiwa kujeruhiwa na chupa kichwani na wala hakutaka waadishi wakutane na askari huyo.

error: Content is protected !!