June 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea Urais Chuo cha mipango atekwa

Spread the love

Uongozi wa chuo cha Maendeleo Vijijini (MIPANGO) umelalamikiwa na baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho kwa kushiriki vitendo vya  kumteka mgombea urais wa serikali ya wanafunzi,Bonifece Mmbando na kumsababishia kushindwa kuzindua kampeini, anaandika Dany Tibason

Mmoja wa wanachuo akizungumza na MwanaHALISI online Paul Mashenene, alisema inashangaza kuona uongozi wa chuo kufanya kitendo cha kumteka mgombea huyo ambaye aliweza kupitia hatua mbalimbali za mchakato wa uchaguzi.

Mashenene alisema kwa mujibu wa katiba ya nchi pamoja na katiba ya Miso mgombea huyo aliyetekwa na mlezi wa wanafunzi ili asizindue kampeini zake ni kitendo cha kulaaniwa na cha kuvunja katiba.

Alisema wakati wa mchakato wa kuwatafuta wagombea urais yalitokea majina 8 ambapo mchujo ulipita na kuwapata wagombea 5.

Shenene alisema mchujo huo kupitia katika tume ya uchaguzi ilipitia tena mchujo huo na kuyapitisha majina 3 ambapo ambapo jina la mgombea urais Bonface Mmbando lilipitishwa.

Alisema kitendo cha uongozi kumteka mgombea huyo na kumfungia ndani katika ofisi ya mshauri wa wanafunzi ni kitendo cha ubakaji wa demokrasia.

Alisema hatua zote zilizofanywa na tume ya uchaguzi iliweza kupitisha majina ya wagombea hadi kufikia hatua ya kuwabakisha wagombea watatu na kati ya hao hakuna mgombea hata mmoja ambaye aliweza kuwekewa pingamizi.

Kwa upande wake mjumbe wa tume ya uchaguzi, Mtani Manyama,alisema anashangazwa na uongozi wa kumfungia mgombea huyo asifanye uzinduzi wa kampeini.

“Kimsingi mchakato wa uchaguzi ulifanyika vizuri,na hatua zote zilifuatwa na hakuwepo na pingamizi la aina yoyote hadi kufikia kati hatua ya tatu bora, lakini jambo la kushangaza ni pale ambapo uongozi wa chuo umefikia hatua ya kumteka mgombea huyo na kumfungia katika ofisi tangu saa 10 hadi 12 wakati wa kumaliza uzinduzi wa kampeini.

Kwa upande wake makamu wa mgombea Prosper Kadumage, alisema anashangazwa na uongozi wa chuo kuingilia uchaguzi wa serikali ya wanafunzi pamoja na kuingilia tume ya uchaguzi.
Kadumage alisema kitendo cha ofisi ya Mshauri wa wanafuzi kumteka mgombea huyo na kumfanya ashindwe kuzindua kampeni kwa madai kuwa mgombea huyo hana sifa ni kitendo cha kubaka demokrasia kwa kiasi kikubwa.

“Sasa mimi hapa sielewi tunafanya nini kwa maana tumepitia taratibu zote na tume ya uchaguzi imefanya kazi yake vizuri sana pamoja na hayo hakuna hata mwanafunzi au mgombea yoyote ambaye ameweza kutoa pingamizi jambo la kushangaza leo asubuhi(juzi) tunaona tanzago kuwa mgombea urais Boniface Mmbando hatakiwi kuzindua kampeini na hana sifa huu ni utawala wa aina gani” alihoji Kadumage.

Mwandishi wa MwanaHALISI online alishuhudia ofisi ya Mshauri wa wanafunzi wa chuo cha Mipango Macarius Mushi ambapo alikuwa wamefungiwa mgombea huyo ikiwa na watu lakini mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.

Mara mlango wa ofisi hiyo ulikuwa ukifunguliwa na na kufungwa kwa ndani mara tu pale ambapo ulikuwa ukigonga kutaka kuingia ndani au kusukuma mlango huo.

Kwa upande wa kaimu mkuu wa chuo cha Mipango, Dk.Frank Awashi alipotafutwa ili aweze kuzungumzia suala hilo aligoma kutoa taarifa hizo huku akiwashutumu mwandishi wa habari hizi kuwa kwanini amekwenda chuoni hapo bila kutoa taarifa.

Hata hivyo alipoombwa kueleza kinachoendelea juu ya tuhuma za mlezi wa wanafunzi kumfungia ndani mgombea urais katika serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, alisema yeye hajui jambo lolote na anasubiri kupatiwa taarifa kutoka kwa waliopo chini yake.

“Mimi sijui kitu chochote na iwapo nitapata taarifa yoyote kuhusu kile kinachoendelea nitawajulisha, lakini mambo hayo yana taratibu zake na mimi sitaki kuzungumzia jambo lolote lakini nashangaa sana kuona kijana huyo anavyokuwa na nguvu hadi kufikia hatua ya kuviita vyombo vya habari”alisema Mkuu wa chuo.

Uzinduzi wa kampeini kwa ajili uchaguzi wa rais wa serikali ya wanafunzi zilizinduliwa juzi ambapo uchaguzi unatarajiwa kufanyika leo.

Hata hivyo mgombea urais Boneface Mmbando pamoja na wapambe wake wanakusudia kwenda mahakamani kwa ajili ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi kwa madai kuwa haki hazikutendeka ikiwa ni pamoja na kumnyima mgombea huyo fursa ya kuzindua kampeini.

error: Content is protected !!