July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea udiwani Mikocheni aahidi neema

Spread the love

MGOMBEA udiwani Kata ya Mikocheni kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kimei Bethel (Mama Langa) ameahidi kuimarisha upatikanaji wa huduma iwapo atachaguliwa kuongoza kata hiyo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kimei ametoa ahadi hiyo jana wakati wa kampeni ya mtaa kwa mtaa iliyofanyika katika kata hiyo, Jijini Dar es Salaam.

Amesema atahakikisha anakabiliana na kero za maji, elimu, uchafu, afya, ajira kwa vijana na ukosefu wa maeneo ya michezo katika Kata ya Mikocheni.

“Ili kuondoa kero hizo, nikichaguliwa nitashirikiana na wananchi katika kusimamia mapato na matumizi ya fedha za maendeleo, kuwakilisha wananchi katika vikao vya maamuzi, kuimarisha ushirikiano na mahusiano ya wananchi ndani ya kata bila kujali itikadi ya vyama wala dini,” amesema Kimei.

Pia, amesema atakuwa mstari wa mbele kukemea na kupinga vitendo vya rushwa, unyanyasaji wa kijinsia na matendo yote maovu.

“Ninaomba ridhaa ya kuwa diwani wa Kata ya Mikocheni kupitia tiketi ya Chadema, nikiwa na dhamira moja kuu ya kushirikiana na ninyi kuleta maendeleo katika Nyanja zote muhimu, “ amesema Kimei.

error: Content is protected !!