January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea Udiwani CUF aibeza serikali

Spread the love

MGOMBEA Udiwani kata ya Ipagala, Manispaa ya Dodoma, Damas Thadei kupitia Chama cha Wananchi (CUF) amesema umasikini unaowakumba watanzania hususani wakazi wa Ipagala unatokana na mfumo mbovu wa serikali ya Chama cha Mapinduzi. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mbali na umasikini amesema serikali haina nia njema na afya ya akina mama wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na wazee ndiyo maana hawapatiwi matibabu stahiki.

Thadei alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika kata hiyo.

Amesema serikali ya CCM inawaandaa watanzania kwa kuwatumainisha kuwa watakuwa na maisha bora kumbe wanufaika wenye maisha bora ni kikundi cha watu wachache.

“Serikali ya sasa siyo ile ya Mwalimu Nyerere ambapo wazee walikuwa wakipatiwa matibabu bure na elimu kutolewa bure na ikumbukwe kuwa hata viongozi walikuwa wakitibiwa hapa nchini.

“Kwa sasa wazee wanadanganywa kwa madai watatibiwa bure lakini cha ajabu wanapokwenda hospitali wanaambiwa wakanunue madawa sasa hapo kuna faida gani ya kuutangazia umma kuwa matibabu ni bure kwa wazee.

“Imefika hatua hata familia zisizo na uwezo zinaogopa kupata watoto kwani mama akipata mimba baba anaanza kupata wasiwasi ni jinsi gani ataweza kumtibia mke wake kwa maana imefikia hatua hata kadi za kliniki zinauzwa licha ya kuwa zimeandikwa kuwa haziuzwi,” amesema Thadei.

Akinadi sera zake mgombea huyo amesema iwapo atachaguliwa kuwa diwani atahakikisha anaibana halmashauri ijenge zahanati katika kata hiyo ili kuondokana na adha kubwa wanayoipata wananchi wa kata hiyo.

Amesema kata hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo ya ukosefu wa zahanati na kuwafanya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya katika kata ya makole.

“Hapa kwetu wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 14 kufuata huduma za afya ambako nako wanaambiwa hakuna dawa, sasa wakati huo umeisha naomba nichague kwa kushirikiana na serikali inayoundwa na Ukawa tulete maendeleo,” alijinadi.

error: Content is protected !!