ALOYCE Luhega, mgombea udiwani wa Kata ya Nzuguni, jijini Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kusimamia ujenzi wa daraja linalounganisha Nzuguni C na B ambalo endapo atachaguliwa. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Luhega ambaye amekuwa diwani wa kata hiyo kwa miaka mitano iliyopita, ametoa ahadi hiyo leo 21 Septemba 2020 katika shule ya Msingi Nzuguni B, Luhega wakati akiomba kura.
Amesema, daraja linalounganisha Nzuguni C na B, limekuwa kero ya muda mrefu na kwamba, tenda ya ujenzi wa daraja hilo imeishatangazwa, na jumla ya Sh. 600 milioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
“Hii imekuwa kero ya muda mrefu, nitasimamia ujenzi wa lile daraja. Nimepambana kuomba hela katika Baraza la Madiwani, sasa tunaenda kulijenga kwani tenda iliishatangazwa,” amesema.
Pia amesema, kwa kutumia fedha zake, ameweza kujenga madarasa saba yenye thamani ya Sh. 220 milioni hivyo anaomba kipindi kingine ili aendeleze ujenzi wa madarasa mengine katika kata hiyo.

“Waache watukane, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hapa tulipo tunaenda kujenga Shule ya Sekondari, Shule ya Msingi Nzuguni B kwa kuwa, ndio shule ya pili yenye wanafunzi wengi kwa Jiji la Dodoma. Tunaenda kujenga shule nyingine ya Nzuguni C ili kukabiliana na tatizo hilo, nipeni kura niyatimize,” amesema Luhega.
Amesema, vikundi 166 vya kina mama, vijana na walemavu vimeweza kupata mikopo yenye thamani ya Sh. 360 milioni katika kata hiyo.
“Ninachotaka undeni vikundi fedha zipo. Mimi sibabaishwi kwani ndio diwani wa miaka ijayo, walionitukana nawasamehe maana CCM haijui matusi na sintoiweka rehani Nzuguni kwa kuwapa madalali,” amesema.
Leave a comment