July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea ubunge CCM azua utata

Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Amina Mrisho Said akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya nia yake ya kugombea ubunge Jimbo la Kiteto, Manyara. Kushoto ni mume wake, Abeid Omary Hamis

Spread the love

KAMISHNA wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012, Amina Mrisho Said, leo ametangaza nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kiteto, mkoani Manyara. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Hata hivyo, Amina ameacha utata kuhusu aliyegharamia mkutano huo kama ni yeye binafsi ama serikali.

Amina ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mikoa ya Pwani na Iringa, ametangaza nia yake katika Ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo, jijini Dar es Salaam kwamba, atagombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Utata wa nani aliyegharamia mkutano huo unatokana na fomu ya mahudhurio ya waandishi waliohudhuria utangazaji nia huo ambayo ilikuwa imebebwa kwa jina la Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Pia fomu hiyo ilikuwa na nembo ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliyoambatanishwa orodha ya waandishi walioshiriki mkutano huo.

Hata hivyo, taarifa ya kuwepo kwa mkutano huo ilieleza kuwepo kwa ufafanuzi kuhusu masuala ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2015.

Tangazo hilo lililobandikwa katika Ofisi za Habari Maelezo lilisomeka kama ifuatavyo;

“PRESS CONFRENCE IPC – MAELEZO SAA- 5.00 ASUBUHI TAREHE: 8.6.2015 KAMISHNA WA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012 NA KADA WA CHAMA CHA MAPINDUZI HAJJAT AMINA MRISHO SAID ATAONGEA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MASUALA MBALIMBALI KUHUSU UCHAGUZI MKUU UJAO.”

Karatasi ya orodha ya waandishi waliohudhuria mkutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ambao ulitumika kutangaza nia ya Ubunge
Karatasi ya orodha ya waandishi waliohudhuria mkutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ambao ulitumika kutangaza nia ya Ubunge

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya waandishi wengi ambao awali walidhani mkutano huo ungehusu masuala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, badala yake Amina aliyeambatana na mume wake, Abeid Omary Khamis alizungumzia nia yake ya kuwania Jimbo la Kiteto.

Kauli yake inathibitishwa na taarifa yake kwa vyombo vya habari ambayo ameweka sahihi yake ambayo MwanaHALISI Online inayo nakala yake.

“Natumia nafasi hii kutangaza rasmi nia yangu kuwa, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nimefanya uamuzi wa kwenda kujitosa kwenye mchakato wa kuwania nafasi ya ubunge wa jimbo la Kiteto Mkoani Manyara katika uchaguzi wa mwaka huu kupitia Chama Cha Mapinduzi,” amesema Amina huku akinukuu andiko la hotuba yake.

Akieleza kuhusu vipaumbe vyake Amina amesema, atatekeleza Ilani ya CCM pamoja na ahadi za Rais Jakaya Kikwete ambazo hazijatekelezwa, kufanikisha ujenzi wa Chuo cha VETA katika jimbo hilo, kuhamasisha ufugaji wenye tija, ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao na kuwashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 1992, mtumishi wa serikali hapaswi kujishughulisha na masuala ya siasa muda wa kazi za serikali, pia haruhusiwi kutumia mali za umma kwa shughuli zake za kisiasa.

error: Content is protected !!