June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea: Msimchague Ngereja hajatekeleza ahadi

Spread the love

MGOMBEA Ubunge jimbo la Sengerema mjini, kupitia Chama cha United Demokratic Party (UDP), Franscico Shejamabu, amewaomba Wananchi wa jimbo hilo kuacha kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake, William Ngereja. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika viwanja vya Ukuryani, kata ya Nyamatongo jimbo la Sengerema.

Shejamabu amesema CCM imesababisha wananchi wa jimbo hilo waishi maisha duni na yenye dhiki kutokana na ahadi zao kutotekelezwa, hivyo ni vyema wakachukua maamuzi magumu ya kutokichagua chama hicho tawala, uchaguzi ujao.

Amesema kuwa mbunge huyo aliyemaliza muda wake ameshindwa kutatua kero za wananchi ikiwemo suala la maji, miundombinu ya barabara, afya na elimu ambayo alidai wanafunzi walio wengi bado wanakaa chini.

Amesema wananchi wa Sengerema wanapaswa kumuamini na kumupa kura za ndio ili kutatua kutokomeza kero za muda mrefu ambazo CCM imeshindwa kuzitatua na badala yake kimeendelea kutumia kodi zao kwa maslahi yao binafsi.

Shejamabu ambaye alijiunga na UDP baada ya kujiengua CHADEMA kufuatia jina lake kukatwa licha kuongoza katika kura za maoni, amesema muda na wakati wa kukiondoa CCM na watu wake madaraka ni Oktoba 25, 2015 kwa kuvichagua vya upinzani kuanzia madiwani, wabunge na nafasi ya urais.

Amesema CCM kimekuwa ni chama cha manyanyaso kwa wananchi wake na kushindwa kuwatatulia matatizo yao na kumaliza kero ambazo zimedumu kwa miaka 54 ya Uhuru na kusababisha wananchi wake kuendelea kuishi maisha duni.

“CCM ni chama cha kiharamia kisichowajali wananchi, naombeni mnichague mimi na viongozi wote wa UDP tuweze kutatua kero zenu ambazo hawa watawala wameshindwa kuzitatua,” amesema Shejamabu.

Shejamabu alivitaja vipaumbele vyake vikuu ambavyo atavishughulikia endapo atachaguliwa kuwa mbunge ni miundombinu ya barabara, kuimalisha kilimo kwa kufungua viwanda, elimu, afya na suala la uchumi ambalo limeonekana kupanda Sengerema.

error: Content is protected !!