January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea CUF arusha kombora CCM

Spread the love

MGOMBEA udiwani katika Kata ya Sandali iliyopo Temeke, Dar es Salaam kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Khalidi Yahaya amekituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wachache. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Yahaya ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) amesema, chama hicho kimekwapua rasilimali hizo na kujimilikisha kwa manufaa yao na familia zao.

Amesema hayo jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya BMK, Temeke jijini Dar es Salaam.

“Chama Cha Mapinduzi – CCM hakina nia ya dhati ya kuwaletea Watanzania mabadiliko kwa sababu wanajua fika wagombea waliowateua si wema kwani baadhi yao wamekaa kwenye uongozi kwa muda mrefu bila ya kufanya chochote,” amesema na kuongeza;

“Mgombea wao wa udiwani, Abel Tarimo wa kata hii amekaa kwenye uongozi kwa muda wa miaka 15 na hajafanya chochote zaidi ya kula pesa za miradi na kujilimbikizia mali.”

Amesema kuwa, mgombea huyo wa CCM aliyeongoza kata hiyo kwa miaka 15 sasa, hajafanikiwa kupiga hatua yoyote na kwamba, ni wakati kwake kupumzika.

“Kwa muda wa miaka 15, kata hii haina haina maendeleo kama ilivyokuwa hapo awali. Mwanzo kulikuwapo eneo maalumu la soko la wafanyabiashara ndogo ndogo ila soko hilo lilibomolewa kwa lengo la kupisha mradi wa shule na zahanati ambao hadi sasa haujatekelezwa na fedha za mradi huo alizila yeye na mbunge wa CCM Jimbo la Temeke, Abasi Mtemvu,” amesema.

Hata hivyo, ameshutumu viongozi wa CCM kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita tano.

“Mbunge Abasi Mtemvu amekaa madarakani kwa miaka 10 na diwani wake wa kata ya Sandali amekaa madarakani kwa miaka 15.

“Kipindi hicho chote zilitoka fedha za miradi mbalimbali lakini miradi mingi hawakuitekeleza, kama ujenzi wa barabara na kuboresha mifereji, fedha za wajasiriamali takribani milioni 190 hazikuwafikia walengwa na pia wameshindwa kujenga Shule ya Sekondali ya Kata ya Sandali,”amesema Yahaya.

Aliyekuwa mgombea wa kata hiyo kutoka Chadema, Jerome Isihaka na kisha kumwachia Yahaya amesema, alikubali kumuachia mgombea wa CUF bila kinyongo.

“Kama hamjui wenzenu wanapanga njama za kuutafuta ushindi kwa nguvu ili warejee tena madarani waendeleze njama zao za ufisadi, wameandaa bajeti ya mwaka 2015-2016 ambapo wamependekeza diwani atakayeingia anunuliwe gari lenye gharama ya milioni 200,” amesema Jerome.

error: Content is protected !!