July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea Chadema hukumu tatu

Spread the love

MGOMBEA ubunge jimbo la Kilombero, mkoani Morogoro, Peter Lijualikali ambaye ana hukumu mbili anazozitumikia kwa sasa, kesho anatarajiwa kusikiliza hukumu ya tatu katika kesi inayomkabili kwenye Mahakama ya Wilaya Kilombero. Anaandika Charles William … (endelea).

Lijualikali anayegombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anatumikia adhabu ya kifungo cha nje kwa miezi sita na nyingine aliyolipa faini ya Sh. 520,000.

Katika hukumu ya kifungo cha nje iliyosomwa Oktoba 8, Lijualikali alitiwa hatiani kwa kosa la kumtukana Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ifakara, Afuley Mwenga.

Katika hukumu ya kupigwa faini, alitiwa hatiani kwa kosa la kumpiga Mtendaji huyo. Katika kesi inayosubiriwa hukumu kesho Alhamisi, ameshitakiwa kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano yasiyo na kibali.

Akizungumzia mashaka hayo yanayomkabili katika kipindi muhimu cha kutafuta ubunge, Lijualikali amesema, “Unajua mimi nilikuwa Diwani sasa katika kutofautiana na Mtendaji wa Kata ndio nikabebeshwa kesi hizo.”

Amesema wakati anasubiri hatima ya keshi ya tatu, anatarajia kukata rufaa.

Amewatia moyo wananchi akisema wasikatishwe tamaa na mfululizo wa matatizo yanayomkuta, kwani ndio matokeo ya mwanasiasa kuamua kusimamia upinzani nchini Tanzania.

“Ninaendelea na kampeni kama kawaida, hukumu zote mbili hazininyimi sifa ya kugombea wala kunikatisha tamaa, wananchi pia waendelee kuwa imara, nimeshafanya mikutano kwenye Kata zote 19 za jimbo hili… ninarudia katika maeneo ‘korofi’ katika siku chache zilizobaki kufikia uchaguzi mkuu Oktoba 25,” anasema.

Jimbo la Kilombero ni mojawapo ya majimbo ambayo CHADEMA inapewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 2014.

Chadema pamoja na CUF walishinda vijiji 59 dhidi ya 48 vya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Jimbo hilo la Kilombero limegawanywa na kupatikana jimbo jipya la Mlimba anakogombea ubunge Susan Kiwanga wa Chadema akiwakilisha UKAWA.

error: Content is protected !!