July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea CCM amdhulumu meneja wake mamilioni

Spread the love

MGOMBEA Ubunge jimbo la Dodoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde anadaiwa kumdhurumu aliyekuwa kampeni meneja wake, Sospeter Mzungu fedha Sh. 3.6 milioni. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mzungu amesema wakati wa kipindi cha mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, walikubaliana na Mavunde aache kazi katika kituo cha radio cha Ras FM kuwa kampeni meneja wake kwa malipo ya kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza katika uzinduzi wa mkutano wa kampeni za Chadema uliofanyika kata ya kiwanja cha ndege Mzungu amesema Mavunde hafai kuwa mbunge wa Dodoma Mjini kwani ni mtu ambaye haaminiki.

“Nilimwamini sana Mavunde, nilidhani anaweza kuwa kiongozi mzuri lakini nimegundua kuwa ni mbabaishaji.

“Sababu za kutomwamini ni hivi, wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM aliniomba niache kazi ili nimsaidie kumfanyia kampeni na kuratibu shughuli mbalimbali ndani ya mchakato huo kwa makubaliano ya kunilipa milioni 3.6 lakini hadi sasa ameamua kuzizika.

“Jamani wananchi nataka kuwaeleza wananchi kwamba iwapo mtamchagua Mavunde ni wazi Dodoma itaendela kuwa nyuma kimaendeleo kwani ni mtu ambaye ana ahadi nyingi ambazo hazitekelezeki,” amesema Mzungu.

Mbali na hilo amesema Mavunde amekuwa akitumiwa zaidi na Mamlaka ya Ustawishaji makao Makao Makuu (CDA) ili kupanga mipango ya kuwabomolea wananchi nyumba zao bila fidia.

Amesema kamwe Mavunde hawezi kukomesha manyanyaso ya ardhi kwa mji wa Dodoma kwani ni sehemu yake ya ulaji.

Mwanahalisi Online ilimtafuta Mavunde kujibu tuhuma hizo, naye amesema, ni kweli anafahamiana sana na Mzungu na ni rafiki yake, lakini aliyosema hayana ukweli wowote.

“Ni kweli huyo jamaa (Mzungu) nafahamiana naye sana na ni rafiki yangu sana, lakini nashangaa kusikia anatumia majukwaa kusema hivyo, kimsingi nimekuwa naye lakini makubaliano hayakuwa hivyo kama anavyosema,” ameeleza Mavunde.

Hata hivyo Mavunde hakuwa tayari kueleza makubaliano yake na Mzungu yalikuwaje.

Kwa upande wake Mgombea Ubunge jimbo la Dodoma Mjini kwa tiketi ya Chadema, Benson Kigaila amesema kipaumbele chake cha kwanza katika jimbo hilo ni wananchi kumiliki ardhi.

Kigaila amesema wakazi wa Dodoma pamoja na mambo mengine wanayokumbana nayo ni kukosa uhalali wa kumiliki ardhi yao.

Naye mgombea udiwani kata ya kiwanja cha ndege kupitia Chadema, Pompi Mnyarapi amesema akichaguliwa atapambana na tatizo la mfumo wa elimu pamoja na kukomesha michango mbalimbali ambayo wazazi wanachangishwa.

error: Content is protected !!