January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea Chadema amchimba mkwara Chegeni

Spread the love

MGOMBEA ubunge jimbo la Busega mkoani Simiyu, Dk. David Nicas (Chadema), amewataka wagombea wenzake akiwemo Raphael Chegeni (CCM) kuacha kujipatia matumaini ya ushindi na badala yake wanapaswa kufungasha mizigo yao na kuondoka kabla ya Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika Moses Mseti, Busega … (endelea).

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Irunga juzi, mgombea huyo ambaye ameonekana kukubalika kwa vijana na wazee, amesema ni vyema wagombea wenzake wakajiondoa mapema na kufanya shughuli nyingine za kujenga Taifa.

Amesema muda huu ni wa mabadiliko kutokana na wananchi wa jimbo hilo kuchoka na sera na ahadi zisizotekelezeka zilizokuwa zinatolewa na wabunge wa CCM na vyama vingine vilivyowahi kuongoza jimbo hilo.

Amesema kutokana na kujitathmini na kujipima kwa takribani ya miaka 10, ameona anatosha kuongoza jimbo hilo ili kusimamia shughuli za kimaendeleo zilishindwa kutatuliwa tangu miaka 52 ya uhuru wa Taifa hili.

Nicas alivitaja vipaumbele vyake endapo atachaguliwa katika uchaguzi huo, kuwa ni kilimo cha uhakika, elimu ambayo alidai kushuka jimboni humo pamoja na kutatua tatizo la maji linalowakabili wananchi.

“Mkinichagua mimi nitakuwa tofauti na wenzagu walionitangulia, nitakuwa nawashirisha juu ya fedha za mfuko wa jimbo zinafanya kazi gani ama tunapanga zitatue kero gani,” amesema Nicas.

Baadhi ya Wananchi waliofika katika mkutano huo, wakizungumza na gazeti hili wamesema wanataka mbunge mwenye uchungu na jimbo hilo kwani wameshindwa kupata huduma ya maji safi kutokana na viongozi wababaishaji.

“Busega tunataka mbunge makini, mwajibikaji na atakaetatua kero ya maji, miundombinu ya barabara na suala la elimu kwani kielimu tupo chini,” amesema Masanja Daud mmoja wa wananchi hao.

Jimbo hilo ambalo lililokuwa likiongozwa na Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani kwa awamu mbili, ni miongoni mwa majimbo matano, kanda ya ziwa yanayokabiliwa na tatizo maji licha ya kuzungukwa na Ziwa Victoria.

error: Content is protected !!