RAIS wa Tanzania, John Magufuli, amempa siku saba William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amkabidhi hati ya shamba lenye ukubwa wa hekta 5,000, linalomilikiwa raia wa kigeni wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilosa … (endelea).
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumatatu tarehe 29 Juni 2020, baada ya kupokea malalamiko ya mgogoro wa ardhi, kutoka kwa wananchi wa Kibamba, wilayani Kilosa.
Kiongozi huyo wa Tanzania, amemuagiza Waziri Lukuvi aliyekuwepo kwenye msafara wake kumkabidhi hati ya shamba hilo, ili aligawe upya, kisha sehemu yake wapewe wananchi wa Kibamba, kwa ajili ya kumaliza changamoto ya mgogoro wa ardhi.
“Kibamba inaonekana kuna matatizo makubwa na sijawahi kuona mahali kuna matatizo ya ardhi kama hapa, ninawaomba sana, ndugu zangu waziri wangu yuko hapa na nina muamini sana. nishaelekeza ndani ya wiki moja watakuja hapa,” amesema Rais Magufuli
“Kuanzia leo waanze kushughulikia hapa, zile hati au mashamba yanayotakiwa kufutwa atayaleta waziri, nataka kabla ya Jumamosi yafike kwangu kwa mkono na nitasaiini saa hiyo hiyo ili yatekelezwe,” amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsikiliza
Rais Magufuli amesema katika uongozi wake, atahakikisha analinda maslahi ya wananchi wanyonge, pamoja na kuwadhibiti wenye nguvu ambao wamekuwa wanadhurumu haki za wanyonge.

“Mnakodishiwa (mashamba) sababu hati ni za wakubwa, nataka nilale nao hao wakubwa, nimesema siku saba waziri pamoja na mkuu wa mkoa ataleta hati, yale mashamba yakufuta, sababu kwa mujibu wa sheria ardhi iko chini ya rais, na mimi nitaenda na watu wanyonge,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewataka wananchi wa Kibamba, kutumia vyema mashamba watakayopewa.
“Naweza futa nusu au kutokana na mapendekezo nitakayopewa nitayagawa kwenu. Mjipange vizuri kugawiwa kwenu isije kuwa chanzo cha kupigana, mtumie uongozi mlio nao kila mmoja apate kipande, kutakuwa sehemu ya wafugaji na wakulima sababu wote tunategemeana,” amesema Rais Magufuli.
Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi
Leave a comment