December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zitto Kabwe: Kinara wa vurugu ACT-Tanzania

Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo

Spread the love

KAMATI Maalum ya chama cha ACT-Tanzania, kimepitia kwa pamoja azimio la kuwafukuza kutoka ndani ya chama hicho, viongozi wake watatu wajuu, Samson Mwigamba, katibu mkuu, Prof. Kitila Mkumbo, mjumbe wa kamati kuu (CC) na Shaban Mambo, makamu mwenyekiti Bara, huku Zitto Kabwe akitajwa kuwa sababu ya kutimuliwa kwao, anaandika Saed Kubenea.

Akisoma azimio la kufukuzwa viongozi hao, mwenyekiti wa ACT-Taifa, Lucas Kadawi Limbu alisema, Prof. Kitila na Mwigamba wamevuliwa uwanachama kwa kosa la kuanzisha chama kipya ndani ya chama cha sasa.

Limbu amesema, Kitila na Mwigamba wamethibitika kupeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa katiba mpya ya ACT, kisha kuisambaza mikoani, kinyume na katiba iliyopo ya chama hicho; kuchapisha bendera mpya, kadi na nembo.

Aidha, Prof. Kitila na Mwigamba wanatuhumiwa kupokea fedha kutoka kusikukojulikana, ikiwa ni sehemu ya mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa kutoka Akaunti ya Escrow.

Vilevile, Prof. Kitila na Mwigamba wamefukuzwa uwanachama wa chama hicho kwa kukiri kukiingiza katika mkataba wa uendeshaji na kampuni ya kigeni kutoka Senegal na bila chama kufahamishwa.

Taarifa zinasema, mbali na makosa hayo, Prof. Kitila na Mwigamba wamefukuzwa katika chama, kutokana na kushiriki maandalizi ya kufanya “mapinduzi” ya kumwondoa mwenyekiti wa sasa Limbu ili Zitto Kabwe aweze kushika usukani wa chama hicho.

Naye Mambo amevuliwa uwanachama kwa kushindwa kujenga chama; kuendesha majungu na kuwagombanisha viongozi wakuu wa chama hicho na wanachama.

Taarifa zinasema, Shaban Mambo, amekuwa akisikika akisema kuwa “Limbu ni mwenyekiti boya,”na kwamba mwenyekiti halisi anatarajiwa kuwasili “…mapema mwaka huu.”

Prof. Kitila Mkumbo na Mwigamba, walikuwa wanachama wa Chadema. Walifukuzwa katika chama hicho tarehe 19 Machi 2014 kwa tuhuma za “usaliti, kukashifu viongozi wakuu wa chama na uchonganishi.”

Makosa ambayo Prof. Kitila na Mwigamba waliyotuhumiwa nayo ACT-Tanzania, ndiyo hayohayo waliyotuhumiwa wakiwa Chadema.

Zitto, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alifukuzwa Chadema yapata mwaka mmoja sasa, na tangu hapo amekuwa akifahamika kuwa mwanzilishi au “mwanachama wa kimyakimya” wa ACT.

Tayari kuna kambi mbili katika uongozi wa ACT – moja ya wajumbe wanaokubaliana na ujio wa Zitto kuwa mwenyekiti; na nyingine inayotaka Zitto aje akiwa mwanachama wa kawaida.

Kundi la wanachama 11 ndilo linaongoza chama, akiwemo mwenyekiti, makamu wake na katibu mkuu.

Wakati kundi hilo moja likipanga kupangua mipango ya kumsimika Zitto; nao Kitila na Mwigamba wanadaiwa kuitisha “kikao cha Kamati Kuu” chenye lengo la kuwafukuza wale ambao wanapinga “ujio” wa Zitto.

Mtoa taarifa amesema, “Mwigamba ameitisha kikao kinyume cha katiba. Yeye na wenzake wamepanga kuutumia mkutano huo kuwafukuza baadhi ya viongozi; wakiwemo mwenyekiti wa sasa na wale wasiokubaliana nao.”

Amesema, Mwigamba na Kitila wanataka kuteka ATC; wanawagawa wanachama na sasa wanapanga mkakati wa kumfukuza mwenyekiti (Limbu), ili kumkabidhi Zitto chama.

“…hatutakubali kukiacha chama tulichopigania kifie mikononi mwa wahamiaji. Tumejipanga kukabiliana nao,” ameeleza mtoa taarifa.

Mkutano ulioridhia kuvuliwa uwanachama Prof. Kitila, Mwigamba na Mambo, ulihudhuriwa na naibu katibu mkuu (Bara) Leopold Mahona; katibu mwenezi na mwenyekiti wa vijana taifa Grayson Nyakarungu; Ramadhani Sulemani Ramadhani ambaye ni makamu mwenyekiti (Zanzibar); Mselemu Suluhu, naibu katibu mkuu Zanzibar na Dotto Zakayo Wangwe, mwenyekiti wa wanawake taifa.

Tayari barua za kuwafukuza kutoka katika chama hicho na muhutasari wa kikao kilichofikia maamuzi hayo, vimewasilishwa ofisini kwa msajili leo asubuhi.

error: Content is protected !!