October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgogoro ardhi Ngorongoro: Wasomi waiangukia Serikali, wataka meza ya majadiliano 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella

Spread the love

 

BAADHI ya wasomi kutoka Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, wameiangukia Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, iitishe meza ya majadiliano kati ya wananchi na wahifadhi, ili kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 60. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo tarehe 29 Januari 2022, jijini Dar es Salaam, wiki kadhaa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela kutangaza nia ya Serikali kuchukua eneo la ardhi kilomita za mraba 1,500, kutoka katika vijiji vya wilaya hiyo kwa ajili ya matumizi ya uhifahdi na uwekezaji.

Ezekiel Ole Mangy, amedai mpango wa Serikali kutaka kuwaondoa wananchi wanaokaa katika tarafa za Ngorongoro inakiuka sheria kwa kuwa miaka 60 iliyopita waliwekwa kwenye maeneo hayo kisheria na kwa makubaliano maalumu matatu, ambayo ni kuendeleza utalii, uhifadhi na maisha ya watu.

Amedai kuwa, wananchi hao hawakujipeleka wenyewe Ngorongoro, bali walipelekwa na Serikali 1959, baada ya kuondolewa Serengeti ili kulifanya beneo hilo kuwa Mbuga ya Taifa.

“Tunaiomba Serikali iingilie kati suala hili  na kuhakikisha kuona kwamba haki inatendeka. Kwa nini Serikali inashindwa kukaa meza ya mazungumzo na watu  wa Ngorongoro? Hatukuwahi kukaa meza na wanaojiita wahifadi tukashindwa kufikia muafaka, imekuwa ikiandaliwa ripoti mbalimbali na kupelekwa kwa Rais au wizara bila kushirikisha watu wa pale,” amesema Mangy.

Mangy amependekeza mazungumzo hayo yatafute muafaka wa namna shughuli za uhifadhi zitafanyika, pasipo kuathiri maslahi ya wananchi ikiwemo makazi yao.

“Tunaiomba Serikali iingilie kati sisi, tunapenda uhifadhi ndiyo maana zaidi ya miaka 60 ile hifadhi ipo hai, tunapokuja kuzungumza haya mambo yametufika shingoni, tumechoka tunaomba Serikali iingilie kati iitishe meza ya mazungumzo na wahifadhi,”

“Na tukizungumza sio mjadala wa wahifadhi kuondoka Ngorongoro tuzungumze namna bora ya kuendeleza utalii, uhifahdi na maisha ya watu wanaohifahdi Ngorongoro,” amesema Mangy na kuongeza:

“Tunaomba wahifahdi wafute neno kuhamisha Wamasai wa Ngorongoro kutoka pale, badala yake waje na neno tutaendeleza vipi uhifadhi, tunaiomba Serikali ya Mama Samia itusaidie, wahifadhi na Serikali ije ikae meza moja na sisi tuzungumze pamoja kwa vipi tutaifanya Ngorongoro iwepo.”

Naye Mwanafunzi kutoka Chuo cha Mzumbe, Laata Mekusi,  ameiomba Serikali iiache Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), itoe uamuzi wa shauri lililofunguliwa na wananchi wa Ngorongoro 2018, kupinga kuondolewa katika ardhi hiyo.

“2018 maboma yalichomwa moto sababu watu waliendelea kuwepo pale. Mwaka huo ilipelekea wenyeji kufungua jalada la shauri katika Mahakama ya Afrika Mashariki, bado halijatafutiwa ufumbuzi. Tunaiomba Serikali  iipe mahakama nafasi yake ya kushughulikia suala hili ikiwa ni haki yake mahakama itatoa tamko na kama ni haki ya wananchi wapewe ili kuondoa bughudha,” amesema Mekusi.

Naye Kasale Mwaana kutoka Chuo Kikuu cha  St. Joseph, amesema mgogoro huo umesababisha huduma za kijamii zisifikishwe katika maeneo hayo kwa sababu ya uhifadhi.

“Watuambie lini tutapata shule Ngorongoro, sababu kule wakipeleka sasa hivi shule mtu anasema naleta msaada wa kuwajengea shule, mhifadhi kule anasema hataki. Tunashuhidia vingi tumenyimwa, shule tumenyimwa na hospitali kinatolewa kibali hawajengi sababu ni uhifadhi, ina maana uhifadhi unatutesa sisi  wananchi,” amesema Mwaana.

error: Content is protected !!