IMEELEZWA kuwa mgodi wa EBR and Partners maarufu Baraka uliopo katika kijiji cha Lyulu – Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita tangu uanze shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwenye kijiji hicho umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hilo. Anaripoti Paul Kayanda, Shinyanga… (endelea).
Hayo yameelezwa jana tarehe 29 Januari 2023 na Meneja wa mgodi huo Sunday Tumaini alipozungumza na waandishi wa habari waliotembelea mgodi huo.
Amesema kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo kulikuwa na wananchi waliokuwa wanafanya shughuli hizo na kwa kuliona hilo Mkurugenzi wa Mgodi huo akawakatia kipande cha eneo kilichopo ndani ya leseni yake ili nao waendelee na shughuli ndogondogo za uchimbaji kwa ajili ya kujipatia kipato kuliko kuwatimua.
“Mgodi huu umekuwa na tija sana hususani kutokana na uzalishaji wake kwani wananchi wamepata ajira lakini pia Serikali imefaidika na kile kinachotoka hapa,” amesema Tumaini.
Aidha, amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni miundombinu ya barabara na umeme hivyo anaiomba Serikali kuwasaidia kuboresha miundombinu ya barabara na pamoja na umeme ili kufikisha madini yanayochimbwa sokoni.
Ameongeza kuwa umeme utaongeza uzalisha kwa tija na serikali kuendelee kunufaika kutokana na uwekezaji wao kwa kutoa mirahaba na hata wananchi wanaozunguka eneo la mgodi nao wanufaike kupitia mgodi huo.
Katika hatua nyingine wamemshukuru Afisa Madini mkazi (RMO) wa Mbogwe kwa ushirikiano anaowapatia ukiwemo ushauri ambao kimsingi unawasaidia kwenye shughuli zao.
Akizungumzia faida za uwepo wa mgodi huo Tumaini amesema wamesaidia kutengeneza barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka wilayani mpaka katika kijiji hicho ambako kuna uwekezaji wa mgodi.
Leave a comment