August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgeja: Makamba anazeeka vibaya

Spread the love

KHAMIS Mgeja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga amesema, Yusufu Makamba, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM anazeeka vibaya, anaandika Charles William.

Mgeja ambaye aliihama CCM mwaka jana na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Meandendeleo (Chadema) amedai kuwa, yupo tayari kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumchunguza Makamba kwa tuhuma za rushwa na ufisadi.

Madai haya yanakuja ikiwa ni siku mbili mfulululizo tangu Makamba kunukuliwa katika gazeti la Uhuru linalomilikiwa na CCM akimbeza Mgeja kuwa, ni mtu asiyejua lolote kuhusu Katiba ya CCM na kanuni zake licha ya kuwahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya mkoa.

“Mzee Makamba anazeeka vibaya sana, mimi nimekuwa kiongozi wa muda mrefu wa chama chake tena katika ngazi mbalimbali na yeye ndiye aliyekuwa akipitisha jina langu ninapogombea. Alikuwa akilipitisha vipi jina la mtu ambaye hajui chochote?” amehoji.

Katika hatua nyingine Mgeja amesema, Makamba hana usafi wala utimamu wa kushambulia watu kwa tuhuma za ufisadi kwani mpaka sasa yeye ni mtuhumiwa mkuu wa ununuzi wa magari ya CCM zaidi ya 200 mwaka 2010 kwa mfumo uliogubikwa na rushwa.

“2010 tukiwa bado CCM, tulihoji Makamba amefanya vipi ununuzi wa Land Cruiser zaidi ya 200 bila kufuata utaratibu na sheria za manunuzi? Makamba hakuwa na majibu na aliagizwa kuleta taarifa kwenye vikao lakini hadi anaondoka nasi tunaondoka hajatoa taarifa,” amesema Mgeja na kuongeza:

“Takukuru ianze kumchunguza Makamba na ufisadi aliofanya ndani na nje ya CCM, huyu si mtu msafi na hili halina ubishi.

“Hata watu walipokuwa wakilalamikia rushwa ndani ya chama kipindi akiwa katibu mkuu, yeye alikuwa akisema, kutoa fedha si rushwa bali ni kuzidiana vipato.”

Pia amesema kama kweli Makamba anajiamini kuwa ni msafi mbele ya umma, aache kutumia gazeti la chama tawala (Uhuru) kushambulia wapinzani na badala yake ajitokeze katika mdahalo wa wazi dhidi ya Mgeja ili aweze kujibu tuhuma za ufisadi alioufanya akiwa katibu mkuu wa CCM.

“Makamba aje katika mdahalo wa wazi, utawala wake mtu asiye na fedha alikuwa hapati nafasi ya ubunge, udiwani au hata ujumbe wa vikao vya juu pia mzee huyu hana maadili ya uongozi, muulizeni kwa nini Mwalimu Julius Nyerere alimfukuza Ukuu wa Wilaya ya Kibondo,” amesema.

Kuhusu tuhuma za ufisadi ambazo Makamba amenukuliwa akimtuhumu Mgeja pamoja na Edward Lowassa, Mgeja amesema; “tumetoka katika dimbwi la rushwa na sisi ni wasafi, unawezaje kuwa mchafu halafu ni mpinzani na serikali hii ya misifa ikakuacha?.”

Makamba alinukuliwa akimshambulia Lowassa tarehe 23 Julai mwaka huu kuwa ni fisadi na ndiyo maana CCM ilimuondoa katika mbio za urais wa chama hicho.

Hata hivyo, Mgeja amepinga akidai Makamba ndiye muasisi na kinara wa rushwa za ndani ya chama hicho.

error: Content is protected !!