MKURUGENZI wa Kampuni ya Agricultural Pharm, Khamis Mgeja, ameiomba Serikali kutatua changamoto ya huduma za pembejeo vijijini ili kuwaondolea wakulima adha ya kutembea umbali mrefu wa kilomita 60 mpaka 80 kufuata huduma hiyo mjini. Anaripoti Paul Kayanda, Kahama…(endelea).
Mgeja ambaye hivi sasa anajihusisha na masuala ya kilimo baada ya siasa, ameshauri ili kutatua changamoto hiyo ni vyema mawakala kupelekwa hadi vijijini.
Mgeja aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mashamba yake na kushuhudia uvunaji wa vitunguu katika Kijiji cha Nyanhembe Kata ya Kilago Mkoani Shinyanga.
Aidha mkulima huyo na mwanasiasa mkongwe nchini alisema kuwa anaimani kubwa na serikali yake na kwamba itasikia kilio hicho cha wakulima kuletewa mawakala wa pembejeo vijijini.
“Fursa hii ya kilimo ina mchango mkubwa katika pato la Taifa na ajira kwa wananchi kwa hiyo tukijielekeza huku, ama tukajielekeza kwenye uvuvi, tukajielekeza kwenye mifugo pamoja na viwanda Tanzania suala la kujitegemea linawezekana,” alisema Mgeja .
Akizungumzia suala la deni la Taifa mkurugenzi huyo alisema kwamba tumekuwa tukilalamika sana kuwa deni la taifa linakua ni kwa sababu mahitaji ya maendeleo ya nchi ni makubwa sana.
Alisema kama watanzania hawatafanya kazi hatutaweza kulipa, hivyo amewaomba wanaolalamika kuhusu deni la Taifa wachape kazi badala ya kulalamika.
“Ni vizuri watu wakajielekeza kwenye sekta ya kilimo, Uvuvi na sekta ya viwanda ili tutakapokuza pato la uzalishaji nina imani hata deni la Taifa linaweza kulipwa na tukaweza kusimama na tukajitegemea,” alisema.
“Kwa rasilimali hizi tulizojaliwa na mwenyezi Mungu za Madini, ardhi ya kutosha, mito na maziwa ambapo maji ni mengi yanayoweza hata kufanya kilimo cha umwagiliaji pamoja na mbuga za wanyama yakiwemo mapori ya akiba,” alisema mkulima huyo.
Leave a comment