MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameishauri Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuja na mipango endelevu ya kutumia mabonde ya maziwa na mito, kuzalisha maji ya kutosha kwa ajili ya kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na wanahabari, leo Jumanne, jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba amesema nchi ina mabonde makubwa tisa, lakini Serikali imekosa mikakati madhubuti ya kuyatumia katika kuzalisha maji.
“Ukitazama takwimu ya uzalishaji maji na mahitaji ya maji, unakuta uzalishaji ni mdogo kuliko mahitaji. Mfano uzalishaji wa maji wa Dawasa kwa 2021 ilikuwa lita za ujazo milioni 147, wakati mahitaji ambayo yalikadiriwa 2020 yalikuwa lita za ujazo milioni 207 hivyo uzalishaji ulikuwa asilimia 70,” amesema Prof. Lipumba.
Mbali na matumizi sahihi ya mabonde ya maji, Prof. Lipumba ameishauri Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuvuna maji ya mvua na yale yaliyoko chini ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba amemtahadharisha Rais Samia kuwa, kama changamoto ya uhaba wa maji iliyopo sasa haitatafutiwa ufumbuzi hadi Oktoba 2025, wananchi watashindwa kupiga kura kwa sababu ya kutafuta maji.
“Lazima tuwe na mikakati endelevu na Rais anaweza kulijua hili vizuri kabisa sababu ukiwa unaingia 2025 Oktoba, ndiyo uchaguzi unafanyika watu wakiwa na ndoo kichwani wakashindwa kupiga kura kisa wanatafuta maji, hali haitakuwa nzuri. Suala hili si dogo ni la maisha ya watu lakini lina athari zake katika hali ya siasa,” amesema Prof. Lipumba.
Leave a comment