April 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mfungwa agomea msamaha wa JPM

Spread the love

MERAD Abraham, aliyekuwa mfungwa katika gereza kuu la Ruanda, mkoani Mbeya, amegoma kutoka gerezani, kufuatia kupata msamaha wa rais. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa kutoka jijini Mbeya zinanukuu vyanzo mbalimbali, ikiwamo kituo cha habari cha Azam, zinasema kuwa Abraham amegoma kuondoka gerezani, kwa maelezo kuwa hana mahali pa kuishi.

“Abraham alikuwa mfungwa katika gereza hili na alikuwa miongoni mwa wafungwa waliopata msamaha wa rais. Lakini kwa bahati mbaya sana, amegoma kuachiwa na katika kuthibitisha kuwa hayuko tayari kurejea uraiani, amejijeruhi usoni kwa kujipiga na jiwe,” ameeleza afisa mmoja wa magereza katika gereza hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mfungwa huyo, ameomba kuhamishiwa kwenye gereza kuu la Ukonga, lililopo jijini Dar es Salaam. 

MwanaHALISI limeelezwa kuwa Abraham alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani, kutokana na kupatikana na hatia ya ubakaji. Hadi jana alikwisha tumikia miaka 19 gerezani.

Kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja siku moja tangu Rais John Pombe Magufuli, kutangaza msamaha kwa wafungwa  5,533, walioko magerezani nchi mzima.

Rais Magufuli, alitangaza msamaha huo jana tarehe 9 Desemba 2019, kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika.

Abraham ni miongoni mwa wafungwa 70 waliokuwemo katika gereza la Ruanda, ambao walinufaika na rais. Anatarajiwa kutolewa kesho.

Katika hatua nyingine, Kameshna Msaidizi wa Jeshi la Magereza mkoani Ruvuma, Richard Nyivwe amesema, mfungwa mmoja aliyefahamia kwa jina la Treson Manyika, amefariki dunia baada ya kupewa msamaha wa rais.

Kamishna Nyivwe amesema, Manyika alikuwa miongoni mwa wafungwa 181 katika gereza la Mahabusu la Songea, mkoani Ruvuma. Alifariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Alisema, “lakini kuna mfungwa mmoja, anayeitwa Treson Manyika, amefariki dunia. Manyika alikuwa miongoni mwa wafungwa 181, walionufaika na msamaha wa rais, kutoka kwenye gereza hili.”

Ameongeza, “Manyika ameaga dunia usiku wa kuamkia leo.

Kwa maana hiyo, wafungwa ambao wametoka rasmi gerezani leo, wamekuwa 179, baada ya mwingine mmoja kuachiwa baada ya kushinda rufaa yake. 

Amesema, anachukua nafasi hiyo ya kupitia mkutano wake na waandishi wa habari, kumuombea kwa Mungu, ndugu Manyika amuweke pema peponi.
error: Content is protected !!