Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mfungua jalada la kesi aeleza walivyomnasa Mbowe
Habari za SiasaTangulizi

Mfungua jalada la kesi aeleza walivyomnasa Mbowe

Spread the love

 

MKAGUZI wa Polisi, Tumaini Swila (46), amedai aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Kingai, alimuagiza asiandike jina la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika jalada la kesi dhidi ya tuhuma zinazomkabili, ili kutunza siri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Inspekta Swila ametoa madai hayo leo Ijumaa, tarehe 4 Februari 2022, akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Ni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021, inayomkabili Mbowe na waliokuwa makomando wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mkhammed Abdillah Ling’wenya.

Wanashtakiwa kwa mashtaka sita ya ugaidi, wanayodaiwa kufanya kati ya Julai na Agosti 2020, ikiwemo kupanga kuwadhuru viongozi wa Serikali, kufanya maandamano yasiyo na kikomo, kuchoma vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu lengo kuzua taharuki na kuifanya nchi isistawalike.

Inspekta Swila amedai, kama jina la Mbowe lingekuwepo katika jalada hilo, taarifa hiyo ingevuja na kumfikia kitendo ambacho kingeweza sababisha asitishe mipango hiyo.

Inspekta Swila anadai , alifungua jalada la uchunguzi tuhuma hizo tarehe 14 Julai 2020 kisha jalada la kesi alilifungua tarehe 18 Julai mwaka huo, baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Boaz ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Mahojiano kati ya Wakili Kidando na Inspekta Swila yalikuwa kama ifuatavyo;

Kidando: Tarehe 14 Julai 2020 ulikuwa wapi?

Shahidi: Tarebe 14 Julai 2020 nilikuwa katika Ofisi za DCI, ndipo nikapokea simu kutoka kwa katibu aliyeko ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), akinitaka nifike ofisini kwa mkurugenzi, wakati huo alikuwa Afande Robert Boaz.

Boaz aliniambia nipokee maelekezo kutoka kwa ACP Kingai akinitaka kufungua jalada la uchunguzi.

Maelekezo hayo alinipa tayari akiwa ameandika kwenye karatasi nayo ilikuwa inaeleza kuwa, mnamo tarehe 14 Julai 2020, majira ya saa 2.30 asubuhi Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Robert Boaz, amepokea taarifa kutoka kwa Luteni Denis Leo Urio za uwepo wa kundi linaloratibiwa na Freeman Aikaeli Mbowe la kutaka kufanya vitendo vya uhalifu.

Ambavyo ni kulipua vituo vya kuuzia mafuta, kuchoma masoko moto pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kufanya maandamano nchi nzima yasiyokuwa na kikomo na kuwadhuru viongozi mbalimbali wa Serikali.

Kwa lengo la kuleta taharuki nchini na kuifanya nchi isitawalike. Matendo hayo yalipangwa kufanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya Arusha na Kilimanjaro.

Kidando: Elezea nini kiliendelea.

Shahidi: Baada ya kunipa maelezo hayo alinitaka nifungue jalada nipeleke kwa DCI, nilienda moja kwa moja mpaka ofisi ya kutunza nyaraka za uchunguzi.

Ambayo ni ofisi ya mhadhini namba moja ya makao makuu ya upelelezi, nilichukua kitabu hicho na kufungua.

Niliweza kufungua jalada la uchunguzi lenye kimbukumbu namba CID/HQ/EE/60/2020.

Kidando: Elezea taratibu za kufungua jalada baada ya kuchukua kile kitabu?

Shahidi: Kitabu hicho ukifungua, taarifa inaonesha tarehe ya kufungua, muda, jina la mfunguaji, jina la mlalamikaji na taarifa yenyewe .

Kidando: Mlalamikaji alikuwa nani?

Shahidi: Malamamikaji alikuwa DCI

Kidando: Mlalamikiwa alikuwa ni nani?

Shahidi: Mlalamikiwa alikuwa Freeman Aikaeli Mbowe.

Jalada nililipeka kwa DCI, siku iliyofuatia tarehe15 Julai 2020, majira ya saa 5 nikiwa ofisi ya DCI, nilikabidhiwa jalada hilo la uchunguzi.

ACP Kingai akaendelea kuwasiliana na mtoa taraifa ili aweze kumtafutia watu ambao waalikuwa wanahitajika na Mbowe kwa ajili ya utekelezaji wa vitendo vya uhalifu.

Lakini katika maelezo hayo akaendelea kueleza kwamba endapo atawapata watu hao, awape tahadhari ya kutoa taarifa ya vitendo vya uhalifu ambavyo wataenda kukutana navyo huko.

Kidando: Kwa mujibu wa maelezo hayo nia hasa ilikuwa ni nini?

Shahidi: Nia hasa ilikuwa ni kutafuta taarifa za kuwajua watu ambao wanashirikiana na Mbowe, kutaka kufanya vitendo hivyo vya kigaidi.

Na zaidi katika hao watu watakaokuwa wamepatikana waweze kuzikusanya hizo taarifa kwa ajili ya kuzifikisha kwa Intelgence Urio, kisha yeye azifikishe kwa ACP Kingai

Akanitaka nikafungue jalada la kesi katika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam.

Kidando: Unamaanisha nini kufungua jalada la kesi kwa mujibu wa maelekezo aliyokupa ACP Kingai?

Shahidi: Ni jalada ambalo linafunguliwa tofauti na lile jalada la uchunguzi na linafunguliwa katika vituo vya polisi

Kidando: Baada ya maelekezo hayo ulifanya nini?

Shahidi: Baada ya kufungua jalada hilo, niliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Ilala, ili jadala hilo liweze kuhamishwa kwenda ofisi ndogo ya DCI Dar ea Salaam.

Kidando: Baada ya hapo ulifanya nini?

Shahidi: Niliweza kwenda Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam na kufungua jalada hilo, kama alivyonielekeza ACP Kingai kufungua jalada la kula njama za kutaka kufanya vitendo vya kigaidi

Kidando: Sasa ya unasema ukaenda kufungua jalada la kula njama za kutaka kufanya vitendo vya kigaidi, hebu elezea shughuli hiyo uliitekelezaje ?

Shahidi: Niliweza kufika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na kufungua jalada hilo ambavyo kama nilivyokuwa nimeelekezwa na ACP Kingai.

Mlalamikaji ni DCI Boaz na jalada hilo aliliekekeza kufungua kuwa, mnamo mwezi kati ya Mei na Julai 2020 kuna kundi la watu wamepanga kufanya vitendo vya kigaidi, katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa lengo la kuleta taharuki nchini na nchi isitawalike

Aidha nilifungua taarifa hiyo kufuatia maelekezo ya ACP Kingai ambaye alitaka nisiandike jina la mtuhumiwa Freeman Mbowe katika taarifa hiyo, ili kuepusha uvujaji wa taarifa.

Kwani kama jina lake lingekuwepo katika taarifa hiyo, angeweza kujua na kusitisha utekelezaji wa mipango aliyokuwa amepanga pamoja na wenzake

Baada ya jalada kufunguliwa lenye kumbukumbu namba CD /IR/ 2097/2020, nilimjulisha aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, kwa wakati huo alikuwa Fadhili Bakari, Mralibu wa Polisi.

Ya kwamba jalada lenye kumbukumbu namba hizo linatakiwa kuhamishiwa Ofisi ya Mpelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, makao makuu ndogo Dar es Salaam.

Kidando: Baada ya kumjulisha Bakari ulifanya nini?

Shahidi: Niliondoka na kuendelea na majukumu mengine

Kidando: Elezea sasa baada ya siku hiyo ya tarehe 18 Julai uliyopewa maelekezo na ACP Kingai ufungue jalada la kesi, kitu gani kingine kiliendelea kuhusu hilo jalada?

Shahidi: Mnamo tarehe 27 Julai 2020, nikiwa ofisi ndogo ya makao makuu ya upelelezi Dar es Salaam, nilipokea jalada lenye kumbukumbu namba CD/IR/2097/2020, lenyw kosa kula njama za kutaka kufanya vitendo vya kigaidi.

Jalada hilo lilikuwa limetolewa malekezo na Afande Kamishna wa Polisi, Robert Boazi akatoa maelekezo kwa Afande ACP Kingai pamoja na mimi, akitutaka tuendelee na upelelezi wa kosa hilo

Kidando: Kitu gani kilikuwa kinaendelea baada ya kupoeka maelekezo hayo?

Shahidi: Niliweza kumjulisha ACP Kingai kuwa nimepokea kwa niaba yako jalada na mimi msaidizi wako

Kidando: Baada ya kujulisha ACP Kingai, nini kiliendelea?

Shahidi: Aliniambia yeye anaendelea na ufuatiliaji kwa kuwasiliana na mtoa taarifa atanipa malekezo ya nini cha kufanya.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!