March 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mfumuko wa bei waongezeka kwa 3%

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii katika Idara ya Takwimu nchini, Ephraim Kwesigabo

Spread the love

MFUMUKO wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018 umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2018. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Sensa na takwimu za Jamii kutoka ofisi ya taifa ya takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Kwesigabo alisema kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka  ulioishia novemba 2018.

“Kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Disemba 2018 ukilinganishwa na ule wa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2017,” alisema.

Aidha alisema kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Disemba 2018 umeongezeka hadi asilimia 1.0 kutoka asilimia 0.4 iliyokuwa mwezi Novemba 2018.

Alisema mfumuko wa bei wa bidhaa sizizo za vyakula kwa mwezi Disemba 2018 umeongezeka hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 2.8 ilivyokuwa mwezi Novemba 2018.

“Baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa mwezi Disemba 2018 ni pamoja na nyama kwa asilimia 4.6, samaki wabichi kwa asilimia 8.5, dagaa kwa asilimia 26.2,matunda kwa asilimia 4.3 na mbogamboga kwa asilimia 8.5″alisema Kwesigabo.

Aliongeza kuwa baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwezi Disemba 2018 ni pamoja na vitambaa vya kushona nguo kwa asilimia 2.1, nguo za kiume na za kike kwa asilimia 6.1, nguo za watoto kwa asilimia 3.0, sare za shule kwa asilimia 3.1.

Pia alisema kuwa viatu vya kiume kwa asilimia 5.5, vifaa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba kwa asilimia 9.1, mafuta ya taa kwa asilimia
18.4, mkaa kwa asilimia 12.3, dizeli kwa asilimia 27.6, petroli kwa asilimia 10.8 na huduma ya malazi kwa asilimia 6.8.

Adha alisema kuwa wastani wa mfumuko wa bei wa taifa kutoka Januari hadi Disemba, 2018 umepungua hadi asilimia 3.5 kutoka wastani wa asilimia 5.3 ilivyokuwa mwaka 2017.

“Wastani huu wa mfumuko wa bei wa mwaka wa asilimia 3.5 ndiyo wasatani mdogo kabisa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita”alisema.

Alisema kupungua kwa wastani wa mfumuko wa bei wa taifa kulichangiwa hasa na kupungua kwa kasi ya bei za bidhaa za vyakula.

“Wastani wa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula umepungua hadi
asilimia 3.7 mwaka 2018 kutoka asilimia 9.6 mwaka 2017″alisema.

Hata hivyo alisema kuwa mfumuko wa bei kwa mwaka uliishia mwezi Disemba 2018 nchini Kenya umeongezeka hadi asilimia 5.71 kutoka asilimia 5.58 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2018 na Uganda umepungua hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2018.

error: Content is protected !!