MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2018 umepungua kutoka asilimia 3.4 mwezi Juni, 2018 hadi kufikia asilimia 3.3. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).
Takwimu hizo zimetolewa leo tarehe 9 Agosti, 2018 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo alipokuwa akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai mwaka huu.
Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kumetokana na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mihogo, maharagwe na matunda jamii ya machungwa.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula, ambapo bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Julai, 2017 na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 9.5, mtama kwa asilimia 17.8, unga wa mihogo kwa asilimia 14.1, matunda jamii ya machungwa kwa asilimia 22.2, maharagwe kwa asilimia 5.8 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.5,” amefafanua Kwesigabo.
Kwesigabo ameeleza kuwa, ni zaidi ya miaka 15 tangu itokee tarakimu kama hiyo ya mfumuko wa bei ambayo iko vizuri kwa uchumi wa nchi.
Leave a comment