August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mfumo wa elimu Tanzania kufumuliwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adlof Mkenda

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imeanza mchakato wa kufanyika kwa mabadiliko makubwa ya sekta ya elimu ikiwemo kuipitia upya Sera ya Elimu ya mwaka 2014. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Lengo ni kukusanya maoni ya wadau mbalimbali ndani na nje ya Serikali ili kuwa na mfumo bora na madhubuti wa elimu utakaowezesha kuwa na wahitimu bora kwa ngazi zote za msingi, sekondari na elimu ya juu.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, tarehe 9 Machi 2022, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adlof Mkenda wakati akielezea mafanikio ya wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia atatimiza mwaka mmoja tarehe 19 Machi 2022 akiwa madarakani, baada ya kupokea kijiti kilichoachwa na mtangulizi wake, John Pombe Magufuli ambaye alifariki dunia 17 Machi 2021, Hospitali ya Mzena iliyopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Profesa Mkenda amesema, katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia amefanya mambo mengi “ambayo sisi tunaona kabisa yanaacha alama. Kitendo cha kusema kila mtoto mwenye fursa ya kwenda shule aende ni jambo kubwa sana. Yawezekana tusione faida leo ila kesho tutaiona.”

Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuelezea kile kinachofanyika sasa cha kuipitia upya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambayo tangu ilipozinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete 13 Februri 2015, imeshindwa kutekelezwa.

Marehemu Benjamin Mkapa

Profesa Mkenda amesema, kuna timu imekwisha kuanza kufanya kazi ipo mkoani Morogoro ikiipitia sera hiyo kuangalia kwa hali ilivyo sasa inaweza kutekelezwa na nini kiboreshwe.

“Rais wetu, alihutubia Bunge alisema tuboreshe elimu yetu kwa kuangalia mitaala yote iliyopo na kinachofundishwa kinaendana na mahitaji ya sasa, kama Rais amesema hadharani na ameendelea kusisitiza kwa vikao vya ndani, kwa nini tusitekeleze dhamira yake,” amesema Profesa Mkande

“Maagizo ya Rais anataka kuona mageuzi makubwa ya elimu ili kuongeza ubora na kufanya wahitimu wanakuwa bora. Tunafurahi kuona wadau wakizungumza kuona kiu ya mageuzi yanafanyika na sisi tumekwisha kuanza kuna timu ipo Morogoro inapitia sera na mitalaa ili kuandaa rasimu,” amesema

Profesa Mkenda amesema, katika kongamano litakalofanyika Mei mwaka huu, “tunataka tuje na rasimu kabisa pale, ili wadau waweze kuijadili na kuitolea mawazo na sisi tutafurahi sana wadau wakishiriki kikamilifu na tunaahidi sisi kama wasimamizi wa wizara tutayachukua ili tuje na kitu kimoja shirikishi.”

Amesema, kumekuwa na mjadala je, elimu msingi iwe miaka saba au kumi, “kigugumizi cha utekelezaji wake hasa sera ya elimu ilikuwa gharama, sasa mimi mchumi, tunaangalia hizo gharama ni zipi na mwisho mimi naamini tutakuwa na mfumo mzuri wa elimu kwa ngazi ya chini hadi chou kikuu.”

Profesa Mkenda alisema, kongamano hilo la siku mbili au tatu, “halitaishia hilo tu, baada ya hilo tutakuwa na makongamano mengine mawili au zaidi lengo ni kuhakikisha tunashirikisha watu wote na kikubwa tuwe na mfumo mzuri zaidi.”

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

Anachokisema Profesa Mkanda kuhusu kongamano hilo kinakata kiu ya wadau wengi waliowahi kutoa maoni na ushauri wao kuhusu umuhimu wa uwepo wa mjadala wa kitaifa wa kujadili mfumo wa elimu.

Miongoni mwa walioshauri hilo ni Hayati Benjamin William Mkapa, Rais wa Tanzania wa awamu ya tatu ambaye kwa nyakati tofauti enzi za uhai wake akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) alishauri jambo hilo.

Mkapa alisema kuna janga katika elimu nchini humo na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi wa kitaifa utakaoshirikisha makundi mbalimbali, “tunahitaji kufanya mapinduzi makubwa kwenye elimu.”

Hakuwa Hayati Mkapa pekee kwani hata Rais aliyemfuatia baada yay eye kuondoka madarakani, Jakaya Mrisho Kikwete akiangazia elimu ya Afrika, kuna haja ya kuangalia mfumo wa elimu kwa bara hilo ili kuwa na wahitimu wenye uwezo.

Kikwete alisema hayo Aprili mwaka 2018 alipokuwa akizungumza katika kongamano la ‘Mageuzi ya Afrika Katika Karne ya 21’ lililoandaliwa na Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani na kushiriksiha viongozi mbalimbali wastaafu.

Rais huyo mstaafu kwenye kongamano hilo alikuwa mmoja wa wasemaji wakuu wanne ambaye alisema Afrika inaweza kuwa inapiga hatua katika kuendeleza elimu, lakini inahitaji kuongeza juhudi hasa kutoka elimu ya msingi hadi sekondari.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Kwa kuangalia takwimu, Afrika ni bara la wahitimu wa elimu ya msingi. Ni asilimia 20 ya vijana wanaweza kwenda shule za sekondari. Kibaya zaidi, hata hao wachache wanaofanikiwa kwenda sekondari hawafanyi vizuri,” alisema

Tarehe 10 Januari 2022, Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kilila Mkumbo akizungumzaa bungeni jijini Dodoma alishauri kupitiwa na kupangwa upya kwa mfumo wa Elimu nchini kutokana na mfumo uliopo kwa sasa kuwa na mapungufu mengi.

Profesa Mkumbo ambaye amewahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Elimu alisema, mfumo wa elimu nchini haujasambaa upo “vertical” ambapo ikitokea mwanafunzi amekosea sehemu moja anajikuta ametoka kwenye mfumo hali ambayo husababisha upotevu wa wanafunzi.

Profesa Mkumbo alisema badala ya kushughulikia changamoto za elimu nusunusu ipo haja ya kuupanga mfumo mzima.

“Tupitie na kuupanga mfumo wetu wa elimu na jambo hili siyo geni, mwaka 1982 Rais wa awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere aliunda Tume ya Makweta ambayo ilipitia mfumo wa Elimu na kuja na suluhisho,” alisema Profesa Mkumbo

Profesa Mkumbo alishauri mawaziri wamshauri Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya Rais itakayopitia mfumo wote wa Elimu na kuupanga upya.

“Jambo hili la kugusa tu mtaala wa msingi peke yake na Sekondari peke yake, haiwezi kututoa tunahitaji elimu ambayo itafiti Karne ya 21 na ambayo itatupeleka miaka 20 mingine ijayo na huu ni wakati muafaka maana Dira yetu inaisha mwaka 2025 hivyo hii itatusaidia kwenda sambamba na Dira yetu,” alisema Profesa Mkumbo.

error: Content is protected !!