KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais nchini Tanzania, Mary Maganga ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kuwa na mfumo bora na wa kisasa katika kuchakata majitaka ili kulinda mazingira. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Hayo aliyasema jana Jumapili tarehe 29 Mei 2022 wakati wa ziara yake katika eneo la mifumo ya kuchakata majitaka yanayotoka katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani.
“Hongereni sana kwa mifumo hii mizuri, afadhali na sisi tuna kitu kizuri ambacho tunaweza kujivunia katika suala la uchakataji wa majitaka hapa Dodoma” alisema Katibu Mkuu Maganga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma, Mhandisi Aron Joseph alisema mfumo huu wa majitaka unafanya kazi kwa ufasaha mkubwa katika kuondoa takasumu pamoja na kemikali nyingine zinazoweza kuathiri mazingira.
Mifumo hiyo ya kuchakata Majitaka katika eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) inasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma na inahudumia chuo pamoja na hospitali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Majitaka na Mazingira DUWASA, Mhandisi Daniel Mgunda alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni matumizi yasiyo sahihi kwa watumiaji.
“Watu wengi hawajui matumizi sahihi ya mfumo wa majitaka hivyo wanatupa vitu vigumu kama chupa, nguo, vitambaa na nepi katika mfumo na kusababisha kuziba mara kwa mara,” alisema Mgunda.
Pia, alisema kumekuwa na wizi mkubwa sana wa mifuniko kwa watu wasiokuwa wema ambao mpaka sasa tumekuwa tukipambana nao.
Leave a comment