Monday , 30 January 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Mfumo ETS wa TRA waonesha mafanikio ukusanyaji mapato
Habari Mchanganyiko

Mfumo ETS wa TRA waonesha mafanikio ukusanyaji mapato

Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Herbert Kabyemera
Spread the love

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema, tangu kuanza kwa matumizi ya Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) umeonesha mafanikio makubwa kwa ongezeko la makusanyo ya kodi ya ushuru wa bidhaa na ongezeko la thamani (VAT). Anaripoti Ibrahim Yamola, Dar es Salaam … (endelea).

Mfumo huo unaofanya kazi kupitia App ya Hakiki Stempu kwa mtumiaji anayeweza kuipakua na kuiweka kwenye simu yake ya kiganjani na kujiridhisha uhalali wa bidhaa kwa kupata taarifa kuwa imezalishwa/imeingizwa nchini na nani, lini na wapi.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa, tarehe 25 Februari 2022, jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Herbert Kabyemera alipokuwa akizungumza katika kikao na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Amesema kupitia mfumo wa ETS, kunaiwezesha Serikali kukusanya kodi kwa uhakika kutokana na taarifa zinazopatikana moja kwa moja toka kwenye mfumo, kwa sababu mfumo huo unachakata taarifa na kuziwasilisha kwenda kwenye mifumo ya TRA pasina kuingiliwa na binadamu.

Kabyemera amesema, tangu kuanza kwa mfumo huo kumekuwa na ongezeko la asilimia 93 ya makusanyo ya kodi ya ushuru wa bidhaa na kodi ya VAT kwa maji yanayofungashwa kwenye chupa yanayozalishwa nchini katika kipindi cha kuanzia mfumo wa ETS kwenye bidhaa hizo tarehe 15 Januari 2019.

Amesema, kuna ongezeko la asilimia 30 ya makusanyo ya kodi ya VAT kwa vinywaji laini kama soda vinavyozalishwa nchini katika kipindi tangu kuanza kwa mfumo wa ETS kwenye bidhaa hizo tarehe 1 Novemba 2019.

Aidha, kuna ongezeko la makusanyo ya asilimia tatu ya makusanyo ya kodi kwa bidhaa aina ya bia na ongezeko la asilimia 6.2 kwa bidhaa aina za sigara zinazozalishwa nchini tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo 25 Januari 2019.

“Hadi kufikia Februari mwaka huu, idadi ya wazalishaji wa bidhaa za sigara, vinywaji (pombe na vinywaji baridi) waliokuwa wanalipa kodi TRA wameongezeka kufikia 307 na waingizaji wa bidhaa toka nje kwa bidhaa za sigara na vinywaji (bia, pombe kali, mvinyo na vinywaji baridi) kufikia 122 ukilinganisha na wazalishaji 57 tu wa bidhaa hizo waliokuwa wanalipa kodi kabla ya matumizi ya EFS 15 Januari 2019,” amesema Kabyemera

Kamishna huyo amesema, tangu kuzinduliwa rasmi kwa kampeni hiyo ya hakiki stempu tarehe 14 Februari 2022, jijini Mwanza wananchi wameendelea kuipakua App na kujiridhisha ubora wa bidhaa kabla ya kuzitumia.

Amesema kwa kipindi cha wiki moja wananchi 4,511 wamepakua App ya Hakiki Stempu ikilinganishwa na wastani wa wananchi 200 waliokuwa wamepakua App hiyo kwa mwezi.

Kabyemera ametumia fursa hiyo kuwaeleza wahariri hao kampeni nyingine wanayoendelea nayo ya ‘kamata wote’ ambayo inalenga kuweka msukumo katika matumizi yam ashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD) kwa pande zote mbili za muuzaji na mnunuzi.

“TRA inasisitiza wafanyabiashara kutoa risiti na wananchi kudai risiti kwa kila manunuzi au huduma wanazopata kwa lengo la kila Mtanzania kuchangia kodi,” amesema Kabyemera

Akielezea jinsi App hiyo inavyofanya kazi na walivyojipanga kuhakikisha wanatdhibiti watu kuitumia vibaya, Meneja wa Mradi wa ETS kutoka TRA, Innocent Minja amesema, mtumiaji wa mfumo huo anapoifungua na kuhakiki bidhaa, taarifa zinaonekana moja kwa moja kwa mifumo wa TRA.

Amesema kama bidhaa husika inakuwa imeingizwa kinyemela, mfumo utaonesha na kutoa maelekezo kwamba atoe taarifa na akitoa taarifa wao wanazipata na hatua zinaanza kuchukuliwa haraka.

Minja amewaomba wananchi kupakua App hiyo inayopatikana kwenye simu janja zote na kujiunga kisha kuanza kuitumia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo amewaomba wananchi kuendelea na utaratibu wa kudai risiti kila wanapofanya manunuzi lengo ni kuhakikisha Serikali inakusanya kodi kikamilifu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chongolo asikitishwa na mradi wa Mil 900 kutoanza kutoa manufaa

Spread the loveKATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari Mchanganyiko

Huawei Tanzania yatajwa miongoni mwa waajiri bora kimataifa

Spread the loveKAMPUNI ya Huawei Tanzania imetajwa kuwa mwajiri bora nchini na...

Habari Mchanganyiko

Waziri wa uchumi wa Finland atua nchini, kuteta na mawaziri 7

Spread the loveWAZIRI wa Masuala ya Uchumi wa Finland, Mika Tapani Lintilä...

Habari Mchanganyiko

Asimilia 79 wafeli somo la hesabu matokeo kidato cha nne

Spread the loveWATAHINIWA wa shule 415,844 sawa na asilimia 79.92 ya watahiniwa...

error: Content is protected !!